Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
NI mateso. Ndivyo unavyoweza kusema, hasa baada ya kundi la maharamia linalojishughulisha na bishara ya ‘unga’ nchini Pakistan kuelezwa kumtesa kijana Mtanzania, Adamu Akida.
Kutokana na hali hiyo, timu ya MTANZANIA ilipiga kambi jana katika eneo la Magomeni, Mtaa wa Idrissa, ambako pamoja na mambo mengine, ilifanikiwa kuzungumza na kaka wa Adamu aliyejitambulisha kwa jina la Hemed Abdallah (si jina lake halisi).
Akisimulia mkasa huo, alisema miezi minane iliyopita, Adamu alikwenda kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Juma, na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.
Baada ya kueleza shida yake hiyo, kaka yake huyo (Juma) alimuhoji kama yupo tayari kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi, na Adamu alikubali kufanya kazi ya aina yoyote ili mradi aweze kupata pesa.
“Adamu kwa sasa ameshikiliwa kwa muda wa miezi minane, hatujui kama alikuwa ameingia katika janga hili hadi pale tulipoona video zake katika mitandao ya kijamii. Hapa aliyepo ni baba yake mdogo, Kessy Baharia na baba yake mzazi yupo Bagamoyo Mlingotini, ndiko anakoendelea na maisha yake.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka wakiwa wameambatana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko ana angerudi mwezi wa tisa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni, tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.
Mke wake
Inaelezwa kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.
Kwamba alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.
“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa Adamu anajua kinachoendelea, maana miezi mitatu iliyopita alihama Magomeni na kuhamia Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu anarejea nchini.
“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa hata kupatikana hapatikani, na hatujui amehamia nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema Abdallah.
Serikali ya Mtaa
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Srikali ya Mtaa wa Idrissa, Issa Mpangile, alisema kuwa jana askari kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya baba mdogo wa Adamu.
Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia, ambaye ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo ya mwenyekiti huyo.
Akizungumza kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa wa Idrissa, Kata ya Magomeni.
Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Wakati Adamu anahama Mtaa wa Idrissa, alikuwa bado ni kinyozi na hakuna rekodi kwamba alikuwa anasafiri nje ya nchi,” alisema Mpangile.
Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.
Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba atakwenda kuripoti kituo cha polisi.
Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.
Serikali yahaha
Baada ya taarifa hizo kuripotiwa na gazeti hili jana, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi wanafanya mawasiliano na Serikali ya Pakistan ili kuangalia namna ya kumwokoa Adamu katika mikono ya maharamia hao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba, alisema tayari wamepata taarifa dhidi ya Mtanzania huyo.
“Kwa sasa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa Pakistan tuone namna ya kumtoa kijana huyo katika mikono ya hao watekaji, na tukikamilisha hilo tutatoa taarifa rasmi juu ya jambo hili,” alisema Advera.
Wakati hayo yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kupitia mmoja wa maofisa wa idara ya habari ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema wamepata taarifa ya tukio hilo, na sasa wanafanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.