NA ESTHER MNYIKA,DAR ES SALAAM
MJUMBE wa Baraza Kuu Jumuiya ya Vijana la Chama cha Wananchi (JUVICUF), Khomein Rwihula amemtaka aliyekuwa Kiongozi Mwandamizi wa chama hicho Tanzania Bara, Julius Mtatiro kuacha malumbano katika mitandao ya jamii.
Akizungumza jana na MTANZANIA, Mjumbe wa JUVICUF, Rwihula alisema umekuwapo mvutano unaoendelea katika mitandao ya jamii kwa viongozi tofauti tangu Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kugombea nafasi ya uenyekiti na kurudi kuwa mwanachama.
Alisema Profesa Lipumba alijiuzulu na baada ya muda aliandika barua ya kurudi CUF kwa mujibu wa kifungu cha 117 katiba ya chama.
“Mtatiro amekuwa tofauti kurejea kwa Profesa Lipumba katika chama… ndiyo huo mvutano unaendelea katika mitandao ya jamii huku wengine wakimtaka arudi katika chama na aendelee na uongozi na wengine wapo kati,”alisema Rwihula.
Alisema hali hiyo imesababisha kuwagawanya wanachama wa CUF, viongozi na mashabiki wa chama hicho.
Aliwaomba viongozi hao kuacha mivutano hiyo na badala yake kujenga mikakati ya kujenga chama hicho.