27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kizaazaa ufungwaji wa hoteli

landmark baada

TUNU NASSOR NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema haiwezi kuingilia uamuzi wa wamiliki wa hoteli waliofunga biashara zao na wengine waliobadili matumizi yake katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo imetolewa siku moja baada ya gazeti hili   kufichua kufungwa kwa baadhi ya hoteli jijini Dar es Salaam na nyingine kubadili matumizi yake katika mikoa tofauti.

Hatua hiyo imechukuliwa na baadhi ya hoteli kutokana na kukumbwa na ukata, baada ya Serikali kupiga marufuku taasisi zake kutumia kumbi za hoteli kwa ajili ya semina na mikutano, ili kubana matumizi.

Kaimu Msemaji wa Wizara  ya Fedha na Mipango, Beny Mwaipaja, aliiambia MTANZANIA, Dar es Salaam jana kuwa hatua ya kutotumia kumbi za hoteli inatokana na uamuzi wa Serikali wa kubana matumizi.

“Serikali ilitangaza kubana matumizi kwa kutaka kumbi za wizara zitumike kwa ajili ya mikutano na suala la kukodi ukumbi litafanyika pale inapobidi na si vinginevyo.

“Tunaamini hivi sasa kila mmoja wetu anatekeleza kama anavyosisitiza kila mara Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ingawa kuna baadhi ya watu wameanza kulitafsiri tofauti agizo hilo halali la Serikali,” alisema Mwaipaja.

Alipoulizwa suala la kufungwa kwa baadhi ya hoteli kutokana na kukosekana kwa mikutano na semina za watumishi wa Serikali, alisema suala hilo linawahusu wamiliki wenyewe kwani Serikali haiwezi kujua utaratibu wao walioupanga.

“Pia wapo wanaodai kuwa hata NGO’s  zinaogopa kufanya mikutano kwenye hoteli kubwa kwa hofu ya viongozi kutohudhuria, hiyo ni hofu yao na Serikali haiwezi kuingilia matumizi ya fedha zao,” alisema msemaji huyo wa Wizara ya Fedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Latifa Sykes, ambaye alisema ingawa hajapata taarifa rasmi za kufungwa kwa baadhi ya hoteli hapa nchini,  anaona hatua ya Serikali kuzuia mikutano kufanyika hotelini, inaweza kuchangia wamiliki kushindwa kujiendesha kwa sababu huduma za kawaida za kula na kunywa haziwezi kuwapatia kipato cha maana kama ilivyo kwa kumbi na vyakula.

Wakati hali ikiwa hivyo, uchunguzi zaidi unaonesha kuwa baadhi ya hoteli maarufu jijini Dar es Salaam zimeendelea kufungwa na hata kubadili matumizi ya biashara hiyo.

Wakati hayo yakiendelea gazeti hili  katika ripoti yake ya uchunguzi limebaini kuwa Hoteli kongwe ya Keys iliyopo Mtaa wa Uhuru jijini Dar es Salaam hivi sasa imebadilishwa matumizi na kuwekwa fremu za maduka.

Hoteli hiyo inayomilikiwa na Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema) hivi sasa imezungukwa na fremu za maduka zaidi ya 15 na kuwekwa kibao chenye maneno yanayosomeka: ‘Keys Shopping Center’ ambapo baadhi yake tayari zimekwishapangishwa na biashara zinaendelea.

Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa wafanyabiashara aliyepo jirani na hoteli hiyo, alisema Keys ilibadilishwa matumizi na kuwa eneo la biashara za maduka ambapo aliyekuwa akiendesha biashara ya hoteli ameondolewa na tayari amehamia sehemu nyingine.

Mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema aliyekuwa anaendesha biashara ya hoteli amefukuzwa na mwenye mali baada ya kushindwa kulipia pango.

“Toka hoteli hii ihamishiwe hapa imekuwa ikifanya kazi kila siku ila kwa leo (jana) tunashangaa tumefika hapa na kukuta imefungwa kwa madai ya kudaiwa kodi na mmiliki wa jengo,”alisema.

Msemaji wa Ndesamburo, Basil Lema alipoulizwa kuhusu suala hilo alikiri sehemu ya hoteli hiyo kujengwa fremu za maduka.

“Hoteli ya Keys haijafungwa, bado inaendelea kutoa huduma zake kama kawaida kwa maana ya watu kulala, isipokuwa kulikuwa na eneo la restaurant (mgahawa) na ukumbi mkubwa nje ya jengo pamoja na eneo la kuchomea nyama ndiyo maeneo yaliyojengwa fremu za maduka” alisema Lema.

Kuhusu madai ya kufungwa kwa huduma za hoteli, msemaji huyo alisema awali ilikodishwa kwa Kampuni ya Royal Oven ambao wamemaliza muda wao, hivyo hoteli hiyo imerudi mikononi mwa mmiliki.

Mbali na hoteli hiyo rungu la makufuli limetawala katika Hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Hoteli hiyo ambayo ilikuwa ikipokea wageni mbalimbali ikiwemo kambi ya timu ya Taifa ilifungwa tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa walinzi aliyekuwa akilinda hoteli hiyo, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema. “ Mmliki wa hoteli hii ameiuza kwa mtu mwingine hivyo anasubiri vibali ndipo ifunguliwe tena na bado hajajua ni lini itafunguliwa,” alisema.

Kuhusu wafanyakazi, alisema hatambui walipo na yupo pale kwa ajili ya kulinda magari. MTANZANIA lilishuhudia kufungwa kwa hoteli hiyo ambapo katika geti la kuingilia hoteli hiyo kulikuwa na kufuli na kubandikwa tangazo linalosema. “Hoteli imefungwa kwa muda kwa ajili ya ukarabati”.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa wiki mbili sasa, umebaini kufungwa kwa hoteli maarufu jijini Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani.

Hoteli ambazo zimefungwa kutokana na sekeseke hilo, ni pamoja na Landmark iliyopo Ubungo, ambayo kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu itaanza kutoa huduma za hosteli na JB Belmont ambazo zipo katika majengo ya Benjamin Mkapa lililopo Posta Mpya na nyingine jengo la Golden Jubilee linalomilikiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSPF.

Pamoja na hali hiyo, gazeti hili lilifanya ziara katika baadhi ya hoteli za mkoani Pwani na kukuta hoteli ya Kiromo View ambayo ilizinduliwa Aprili 11, mwaka 2009 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ikiwa imefungwa.

Kutokana na kile kilichoelezwa kuwa makali ya kodi, Januari mwaka huu, hoteli ya JB Belmont ya jijini Mwanza ambayo viongozi wa kitaifa na kimataifa hufikia, imefungwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mkataba kati yake na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wafanyakazi wa hoteli ya Kiromo View, ambaye jina lake linahifadhiwa kwa usalama wake, alisema hatua ya kufungwa kwa hoteli hiyo imetokana na kodi iliyokuwa inadaiwa na Serikali pamoja na kukosa wateja, hasa katika kumbi zake za mikutano.

“Hii hoteli ilikuwa inaendeshwa kwa ubia kati ya mmiliki wake na kigogo mmoja (jina linahifadhiwa), ambaye alikuwa katika utawala wa Serikali ya awamu ya nne. Ilipofika mwanzoni mwa Desemba, walikuja hapa watu wa TRA na kusema wamepokea agizo la Serikali kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

“Kutokana na hali hiyo, tulipata taarifa kuwa TRA walikuwa wanadai kodi kubwa na tangu ilipofunguliwa ilikuwa haijalipwa… na baada ya hapo tu, tuliambiwa kuwa hoteli inafungwa kwa sasa.

“Kama unavyoona, kwa sasa majani yameota, pamegeuka makazi ya mbuzi na kuku. Ila kwa sasa baadhi ya wafanyakazi ambao tupo hapa, tunafanya kazi kwenye hoteli Bagamoyo mjini na kurudi hapa, kwani tunalala na vyumba vilivyokuwa vya wageni ndivyo tunavyoishi sisi,” alisema mfanyakazi huyo ambaye alikutwa hotelini hapo.

Kutokana na hali hiyo, taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA kwamba hivi sasa wamiliki wa hoteli hiyo wapo katika mazungumzo na chuo kimojawapo (jina linahifadhiwa) ili kuweza kugeuza matumizi yake na kiwe chuo kikuu.

Hoteli hiyo yenye majengo zaidi ya 10 na vyumba vya kulala wageni zaidi ya 128, kwa sasa imekuwa ni sehemu ya kujidai kwa wafanyakazi wa eneo hilo, ambao wamekuwa wakilala bila malipo yoyote, huku baadhi yao wakiendelea kudai stahiki zao.

Kwa upande wa hoteli za JB Belmont zilizopo katika majengo ya Benjamin Mkapa na Golden Jubilee jijini Dar es Salaam, nazo zimefungwa huku walinzi wakibaki kuzunguka katika maeneo hayo kulinda mali.

Uamuzi huo wa serikali ya awamu ya tano umezilazimisha baadhi ya hoteli kufunga huku zingine zibadilishwa na kuwa hosteli na vyuo.

Hali ya biashara katika baadhi ya hoteli si nzuri, kwani MTANZANIA ilitembelea hoteli nyingine za Girrafe, Ramada, Landmark Mbezi beach, White Sands, Jangwani Sea breeze na Sea Scape ikielezwa ni ya kusuasua kutokana na wateja kupunguwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles