Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
HABARI wasomaji wa vituko vya bodaboda, kwa wale ndugu zangu Waislamu waliokuwa katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani nawapongeza kwa kumaliza salama.
Nawakaribisha katika safu yetu na kama ilivyo ada tunajifunza kuhusu biashara ya bodaboda inavyokwenda huku ikiwa imeambatana na vituko mbalimbali.
Mtanzania ilifanya utafiti kwa baadhi ya mikoa kuangalia vijana waendesha bodaboda wanapendelea nini zaidi katika kuongeza mbwembwe katika biashara zao.
Kimojawapo ambacho Mtanzania ilikibaini ni maandishi yenye kuvutia katika mapepe ya pikipiki zao.
Kila mmoja anashindana na mwenzake kuweka jina alipendelo ambalo wakati mwingine humjengea umaarufu kupitia maneno hayo katika pepe.
 Dar es Salaam
Baadhi ya vijana katika pikipiki zao walikuwa wameandika kama ifuatavyo:
Kitambi bila Yesu?, Mkanye mkeo bodaboda si yangu, kazi mbaya ukiwa nayo, ukikosa tumaini kula kula tumbo, ukitaka kujua njia ya mkato kula nauli.
Maneno mengine ni; Ukitaka kusahau shida vaa viatu vinavyokubana, mapenzi kipaji si wote wanaojua, usijisifu una mimba msifu na aliyekupa mimba, yatima hadeki, hata bibi alikuwa bikra.
Hivyo ndio vibwagizo vya waendesha bodaboda jijini, ukisoma mwenyewe unacheka kwanza kisha unapanda pikipiki yake kama umevutiwa.
Mtwara
Vibwagizo havikuishia huko tu, Mtwara wanasema kunenepa wakati nakudai ni dalili ya dharau, kunya anye kuku akinya bata kaharisha, ukikosea kujenga utaboa ukikosea kuoa utajuta.
Tabora
Wao wanasema katika mapepe yao kwamba kikubwa pesa ya bosi kwanza, ulifikiri kumwambia baba yako hello kwenye simu ndio heshima.
Morogoro
Dalalila ange ane dibwe yaani mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio, nyuki hakumbatiwi na usiyempenda kaja.
Dodoma
Safari za nje tuachieni sisi, mchezo wa mapenzi hauhitaji hasira.
Kagera
Vijana wanasema kuku kuku jogoo jina, gari bovu linavutwa kwa gari zima.
Wasomaji wa vituko vya bodaboda hizo ni mbwembwe kwa baadhi ya mikoa lakini mikoa yote vijana wanaweka maneno katika mapepe.
Maneno hayo wanayatumia katika maisha yao ya kila siku na yanaashiria kwamba waendesha bodaboda wengi ni vijana.
Yako maneno mengi yanaandikwa yakiwa na maana kwa mwendeshaji wa bodaboda husika kama vile kuandika Jembe katika pepe lake.
Nilipofuatilia nilibaini anajiona mshindi, ni mnywaji mzuri wa viroba na aliwahi kupata ajali akiwa amekunywa viroba.
Kijana alirushwa na gari maeneo ya Mtoni Mtongani lakini alipokuja kuokotwa katika mtaro alikutwa akiwa hana jeraha.
Aliondoka na bodaboda yake hadi Kiwalani, alijiona mzima hakufika hata hospitali japo pikipiki ilikuwa imeharibika sana.
Kila alipokuwa akiulizwa kuhusiana na ajali yake alikuwa anamalizia na kibwagizo ‘mimi Jembe’ ndipo wenzie walipoanza kumuita hivyo.
Kijana anasahau kwamba majeraha yanayoweza kuwa ndani na baadaye yakatokea madhara makubwa hasa kichwani.
Kila aliyeandika anamaanisha nini anachosema hivyo mapepe ya kila bodaboda yana maana kubwa.