Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amewakutanisha Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na baadhi ya wabunge wa upinzani wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao ambao hivi karibuni kupitia kambi yao walitangaza mgogoro na Dk. Tulia ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF).
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli alisema, hivyo ndivyo inavyotakiwa na kueleza kuwa atashirikiana na wabunge wa upinzani, kwani kwake taifa kwanza vyama baadaye.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa mpango wa ugawaji wa madawati 60,000 kwa wabunge wa majimbo 155, ambapo alisema kuwa amefurahishwa kwa kuwaona wabunge hao wa upinzani wakiwa na Naibu Spika katika hafla hiyo.
“Nimefurahi sana kumwona Msigwa, hii ndiyo Tanzania ninayoitaka. Kwa mwelekeo huu tumeanza historia mpya, tuweke masilahi ya Watanzania mbele vyama baadae.
“Tutatue changamoto bila kujali vyama, wanaokaa chini huwezi kujua yupi baba yake anatoka upinzani, anayekaa katika dawati pia huwezikujua.
“…leo (jana) nawaona Tulia na Msigwa wako jirani, hicho ndicho tunachokitaka, nampongeza Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, katika hotuba zake zote za maendeleo. Nawaahidi wabunge wa vyama vyote tuko pamoja kwa ajili ya maendeleo. Sakaya (Mbunge wa Kaliua), usiogope kusema kama katika jimbo lako kuna jambo linahitajika kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Akizungumzia utengenezaji wa madawati, Rais Magufuli alisema kasi iliyotumiwa na SUMA JKT na Magereza kutengeneza madawati 60,000 haikumridhisha japo madawati ni mazuri.
“Hundi ya kutengeneza madawati ilikabidhiwa Aprili 11 mwaka huu, leo (jana) Julai 13 ni miezi mitatu, madawati yaliyotengezwa 60,000, najiuliza kuna makambi mangapi, yapo zaidi ya 10.
“Fedha zipo, watu wa kufanya kazi wapo, hii nayo hairidhishi, JKT na Magereza mjipange vizuri haiingii akilini kutengeza madawati machache hivyo kwa miezi mitatu, chukueni hili kama jukumu la haraka.
“Shilingi bilioni nne nitakazochukua kutoka BoT nitakuwa na shaka kuzielekeza jeshini, kwa spidi hii madawati yatamalizika kutengenezwa mwaka 2017,” alisema.
Kiongozi huyo wa nchi alisema kuwa watengenezaji hao wa madawati walitakiwa kumaliza haraka huku akitaka maelekezo ikiwa uwezo wao umeshia hapo ili aweze kutafuta vijana ambao atawapata kwa kutangaza zabuni.
“Kama uwezo wenu umeishia hapo niambieni, tutafute vijana, lakini hapo nitahitajika kutangaza zabuni, tulizielekeza kazi kwenu sababu hakuna rushwa, nisaidieni kutengeneza madawati,” alisema.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Naibu Spika Dk. Tulia alisema kwa awamu mbili ya madawati hayo yanatakiwa kuwa 120,000 ambapo kwa awamu ya kwanza yamegawiwa katika mikoa mbalimbali.
Alitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam madawati, 5,370, Pwani 4, 833, Morogoro 5,907, Lindi 4,296, Mtwara 5,370, Iringa 3,759, Njombe 3,222, Mbeya 3,759, Songwe 3,222, Rukwa 285, Katavi 2,685, Unguja 32,000, Pemba 1,800 na Tanga madawati 6,444.
Dk. Tulia alisema ugawaji wa madawati wa awamu ya pili utakuwa Septemba 30 mwaka huu, utahusisha kanda mbili ambazo ni mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Ziwa, Kanda ya Kati na Magharibi.
Akishukuru baada ya kupokea madawatiu hayo kwa niaba ya wabunge wote, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alisema wanaunga mkono juhudi hizo na watahakikisha wanafunzi wote nakaa kwenye madawati.
Mbunge huyo alisema Jimbo la Ilala linatarajia kukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda Sh milioni 27 kwa ajili ya madawati ambapo fedha hizo zimetoka katika mfuko wa jimbo.
Katika Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni, wabunge wa upinzani walisusia vikao vyote vilivyoongozwa na Dk. Tulia, kutokana na kile walichodai ni kuburuzwa na kiongozi huyo wa Bunge.