30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Kikwete: Nipo tayari kuitumikia AU

RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete
RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete, amesema hajaandika barua yoyote ya kuomba kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU).

Hata hivyo, alisema yupo tayari kuitumikia Afrika iwapo viongozi wa bara hilo wataridhia na kumteua kuongoza katika nafasi hiyo.

Kikwete alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa tatu wa watafiti wa kujadili maridhiano ya Paris, kuhusu mabadiliko ya tabianchi, alipoulizwa kuhusu jina lake kutajwa kuwa miongoni mwa majina matatu bora yanayopendekezwa kushika nafasi hiyo.

“Tatu bora ya wapi, sipo tatu bora. Lakini inawezekana mtu anaweza kukaa mahali na kuona hawa watatu wanaweza kutufaa, lakini sijaomba.

“Hata kama mtu anafikiria kwamba fulani atatufaa, si mpaka iwe. Hata huko Umoja wa Mataifa wapo wanaonifuatilia kwamba nitafaa, watu wananiambia kwamba ungefaa wewe (yeye), lakini nikawaambia sijaomba.”

Alisema iwapo viongozi wa Afrika watalipendekeza na kuliteua jina lake, yupo tayari kuitumikia Afrika kwa nafasi hiyo.

“Sikilizeni, hapa duniani nimeshafanya kazi kubwa kuliko zote ambazo mwanadamu anaweza kuzifanya, leo hii siwezi kuandika barua ya kuomba kazi.

“Watu wananitaja, ni kweli, lakini sijaomba nafasi ya Katibu Mkuu wa AU, mimi si mgombea, wagombea wapo. Mimi nimesoma, watu wananiombea heri na inshallah Mungu ajalie, lakini katika hili sijaomba.

“Kwenye hili haliwezekani mimi kupata nafasi hiyo kwa sababu sijaomba, na hadi upate lazima uwe mgombea.

“Lakini kama viongozi wa Afrika wataweza kuona ninafaa, nipo tayari kujitolea kwa muda mfupi kuitumikia Afrika.

“Wakiniteua nitakubali, lakini si kuandika barua, siwezi kukimbia na wala kuipa kisogo Afrika. Watu wananiombea kwamba naweza kufaa, sina hakika sana. Lakini pengine naweza kufaa kuitumikia Afrika,” alisema.

Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, alisema ni matatizo halisi na wala si ya kutunga, na yamesababishwa na mwanadamu mwenyewe.

“Tanzania tuna mfano halisi, joto limeongezeka, limeanza kuathiri mfumo mzima wa hali ya hewa, dunia imeharibika mvua haitabiriki, maeneo mengine yanapata ukame na vimbunga vimeongezeka,” alisema.

Alisema zamani siku za mvua kunyesha zilikuwa zinajulikana tofauti na ilivyo sasa.

“Tulijua wazi Machi 15 tunapata masika, Oktoba 15 mvua za vuli, siku hizi hakuna. Mwaka jana vuli hatukupata, mwaka huu Aprili 1 hadi 30 tumepata  masika, wakulima wenzangu mahindi yamebaki bila kuzaa mashambani, tumepata hasara,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles