32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hoteli zatikiswa

Hotel ya Landmark iliyopo Ubungo Riverside iliyogeuzwa kuwa hosteli ya wanafunzi.
Hotel ya Landmark iliyopo Ubungo Riverside iliyogeuzwa kuwa hosteli ya wanafunzi.

* Wamiliki wazigeuza kuwa hosteli, vyuo na nyingine zapingwa kufuli

Na WAANDISHI WETU,

UAMUZI wa Serikali ya awamu ya tano kubana matumizi kwa kuzuia wizara, taasisi na mashirika ya umma kufanya mikutano kwenye hoteli, pamoja na kodi, sasa machungu yameanza kuuma kwa wamiliki wa biashara hiyo.

Kutokana na hatua hiyo, hoteli maarufu zilizopo Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine, zimelazimika kufungwa na huku nyingine zikibadilishwa na kuwa hosteli kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kati.

Mbali na hilo, pia baadhi ya wamiliki wa hoteli hizo wamelazimika kupunguza wafanyakazi kama njia ya kukabiliana na athari za ukosefu wa mapato.

Baada ya kuapishwa na kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi yasiyo ya lazima, ikiwamo kuwataka watendaji wa mashirika ya umma kutofanya mikutano katika kumbi za mahoteli na ikiwezekana wafanyie chini ya miti.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA kwa wiki mbili sasa, umebaini kufungwa kwa hoteli maarufu jijini Dar es Salaam na nyingine mkoani Pwani.

Hoteli ambazo zimefungwa kutokana na sekeseke hilo, ni pamoja na Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam ambayo kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu itaanza kutoa huduma za hosteli.

Kwa upande wa hoteli za JB Belmont zilizopo katika majengo ya Benjamin Mkapa na Golden Jubilee jijini Dar es Salaam, nazo zimefungwa huku walinzi wakibaki kuzunguka katika maeneo hayo kulinda mali.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa walinzi waliokutwa katika maeneo hayo, ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kuwa hoteli hizo zimefungwa kwa muda wa miezi minne sasa.

“Hoteli hii imefungwa kwa miezi minne sasa na hatujui sababu ya kufungwa,” alisema mlinzi huyo.

Kutokana na kile kilichoelezwa kuwa makali ya kodi, Januari mwaka huu, hoteli ya JB Belmont ya jijini Mwanza ambayo viongozi wa kitaifa na kimataifa hufikia, nayo imefungwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya mkataba kati yake na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Alipozungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa NSSF, Yakoub Kidula, alikiri kufungwa kwa hoteli za JB Belmont zilizokuwa zikiendesha biashara katika majengo yao.

Kidula alisema sababu kubwa ya hoteli hizo kufungwa, ni kutokana na mwekezaji huyo kushindwa kulipa kodi ya pango inayokadiriwa kufikia Sh bilioni mbili hadi tatu.

“Ni kweli hoteli za JB Belmont zote za Dar es Salaam na Mwanza zimefungwa kutokana na malimbikizo ya madeni.

“Biashara yake imeyumba, ameshindwa kulipa kodi ya pango, siwezi kutaja kiwango kamili, lakini ni kati ya Sh bilioni mbili au tatu, ni fedha nyingi,” alisema.

Kuhusu kuzuiliwa kwa mali za mwekezaji huyo, Kidula alisema. “Kwanza ‘asset’ (samani) zote ni za kwetu. Tunaamini shirika litapata fedha zake kwani suala hili lipo mahakamani, kwa kuwa wao ni kampuni watalipa,” alisema.

Kwa upande wa hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo, tangu Julai Mosi mwaka huu, uongozi unadaiwa kuwa uliamua kuifunga ili kutafakari namna ya kugeukia biashara nyingine.

Pamoja na kufuatiliwa suala hilo kwa muda wa wiki moja, ilipofika jana waliweka tangazo ambalo linaeleza kuwa kuanzia Septemba mwaka huu, itakuwa hosteli kwa ajili ya wanafunzi.

Mmoja wa wahudumu ambaye alizungumza na gazeti hili, alisema kuwa vyumba vya hoteli hiyo vitatumika kama hosteli kwa ajili ya wanafunzi watakaopanga katika jengo hilo.

Hoteli hiyo maarufu inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja maarufu ambaye pia ni mbunge wa CCM katika Bunge la 11, imelazimika kufungwa huku wakiacha sehemu ya kumbi za chini kwa ajili ya watakaokuwa na mikutano yao.

“Huduma za kumbi za mikutano zitaendelea ila watu watakuwa hawalali hapa, tutawapeleka eneo moja Sinza na kuwaleta hapa asubuhi tu. Na hili ndiyo tumeelezwa na sasa tunajipanga.

“Tulikuwa na wafanyakazi wengi, wapo waliopunguzwa na wachache kubakishwa kwa ajili ya kuhudumia jengo, nyie si mnajua hali ya sasa ilivyo, basi hiyo ndiyo hali halisi,” alisema mfanyakazi huyo.

Alipotafutwa meneja wa hoteli hiyo kwa simu, ambaye alitambulika kwa jina la Omary Mbuly, alikiri kubadili matumizi ya hoteli hiyo, lakini hata hivyo akasema huduma nyingine kama baa na kumbi zitaendelea.

“Ila suala la wafanyakazi siwezi kulizungumzia kwa sababu nami ni mfanyakazi kama mwingine ambaye analipwa mshahara, ninaomba uje kesho (leo) utapata majibu yote. Na kama kuna suala linalohusu kodi, kwa kweli kwangu ni zito kulizungumzia, upo uongozi wa juu wenye uwezo wa kuzungumzia hili kwa undani,” alisema meneja huyo na kukata simu.

Pwani

Gazeti hili lilifanya ziara katika baadhi ya hoteli za mkoani Pwani na kukuta hoteli ya Kiromo View ambayo ilizinduliwa Aprili 11, mwaka 2009 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ikiwa imefungwa.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, ambaye jina lake linahifadhiwa kwa usalama wake, alisema kuwa hatua ya kufungwa kwa hoteli hiyo imetokana na kodi iliyokuwa inadaiwa na Serikali pamoja na kukosa wateja, hasa katika kumbi zake za mikutano.

“Hii hoteli ilikuwa inaendeshwa kwa ubia kati ya mmiliki wake na kigogo mmoja (jina linahifadhiwa), ambaye alikuwa katika utawala wa Serikali ya awamu ya nne. Ilipofika mwanzoni mwa Desemba, walikuja hapa watu wa TRA na kusema wamepokea agizo la Serikali kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

“Kutokana na hali hiyo, tulipata taarifa kuwa TRA walikuwa wanadai kodi kubwa na tangu ilipofunguliwa ilikuwa haijalipwa… na baada ya hapo tu, tuliambiwa kuwa hoteli inafungwa kwa sasa.

“Kama unavyoona, kwa sasa majani yameota, pamegeuka makazi ya mbuzi na kuku. Ila kwa sasa baadhi ya wafanyakazi ambao tupo hapa, tunafanya kazi kwenye hoteli Bagamoyo mjini na kurudi hapa, kwani tunalala na vyumba vilivyokuwa vya wageni ndivyo tunavyoishi sisi,” alisema mfanyakazi huyo ambaye alikutwa hotelini hapo.

Kutokana na hali hiyo, taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA kwamba hivi sasa wamiliki wa hoteli hiyo wapo katika mazungumzo na chuo kimojawapo (jina linahifadhiwa) ili kuweza kugeuza matumizi yake na kiwe chuo kikuu.

Hoteli hiyo yenye majengo zaidi ya 10 na vyumba vya kulala wageni zaidi ya 128, kwa sasa imekuwa ni sehemu ya kujidai kwa wafanyakazi wa eneo hilo, ambao wamekuwa wakilala bila malipo yoyote, huku baadhi yao wakiendelea kudai stahiki zao.

Mwanza

Katika Jiji la Mwanza, pia hali ya biashara ya hoteli imezidi kuwa mbaya kutokana na agizo la Serikali kuzitaka taasisi zake kufanyia semina katika kumbi za Serikali.

Akizungumzia hali ya biashara, mmoja wa wasimamizi wa Hoteli ya Gold Crest, ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini kwa madai kuwa si msemaji, alisema kwa sasa biashara imebadilika sana na hali ya uchumi imekuwa mbaya.

“Zamani tulikuwa na shughuli kwa kiasi fulani, lakini kwa sasa tunapata lakini si nyingi, ila kwa kifupi hali si nzuri kwa biashara ya hoteli,” alisema.

Tanga

Uchunguzi wa gazeti hili katika hoteli za Malindi, Regal Naivera, Mtendele na Mkonge mkoani Tanga, imebainika kuwapo idadi ndogo ya wateja kuliko ilivyokuwa zamani.

Wakizungumza na gazeti hili, mameneja wa hoteli hizo, walisema kuwa kitendo cha kuzuiwa kwa semina kimewaathiri hali iliyosababisha baadhi ya hoteli kupunguza wafanyakazi.

Arusha

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA katika Jiji la Arusha, umebaini kuwa baadhi ya hoteli za kitalii zenye kumbi za mikutano zimeanza kutafakari hatua za kuchukua, ikiwamo kupunguza wafanyakazi kama njia ya kukabiliana na mdororo wa kiuchumi.

Akizungumzia hilo, Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Impala inayomiliki hoteli za kitalii za Impala, Ngurdoto na Naura Spring, Felix Daniel, alikiri kuwa kwa kiasi agizo la Rais Magufuli limeathiri sekta yao.

Hata hivyo alipotakiwa kueleza iwapo tayari wamepunguza wafanyakazi, hakukataa wala kukubali zaidi ya kutoa maelezo ya jumla kuhusu hatua hiyo ya Serikali.

“Sina hakika unalenga nini katika swali lako, lakini hatujapunguza wafanyakazi kwa vile Serikali imeacha kutumia kumbi na hoteli zetu. Hata hivyo hata kama tutapunguza, hiyo si sababu pekee, kwa sababu tulipoanzisha biashara hatukulenga Serikali kama mteja wetu,” alisema.

Manyara

Kwa upande wake, mmiliki wa hoteli ya Freetown Kibaya, Niko Moses, alisema analazimika kufikiria kazi nyingine ya kufanya kufuatia biashara ya hoteli kutolipa na kusababisha hasara.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Latifa Sykes, alisema ingawa hajapata taarifa rasmi za kufungwa kwa baadhi ya hoteli hapa nchini, anaona hatua ya Serikali kuzuia mikutano kufanyika hotelini, inaweza kuchangia kushindwa kujiendesha kwa sababu huduma za kawaida za kula na kunywa haziwezi kuwapatia kipato cha maana kama ilivyo kwa kumbi za mikutano na vyakula.

“Hali hii haitaathiri hoteli pekee, bali hata sekta nyingine, zikiwamo za kilimo, usafirishaji na ajira,” alisema.

Alisema awali wamiliki wa hoteli waliwahi kukaa na serikali ambapo waliainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya utalii, lakini badala ya kuondoa zile changamoto imewaongezea mzigo mwingine wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mkurugenzi huyo alisema japokuwa sekta ya hoteli ilikuwa inalipa vizuri VAT tangu awali, zilikuwa zinatokana na mikutano ya Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO) pamoja na sekta binafsi, ambayo hata hivyo hivi sasa  wanaogopa kufanya mikutano kwa hofu ya viongozi wa Serikali kushindwa kuhudhuria,” alisema Latifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles