TEXAS, MAREKANI
MAUAJI ya maofisa watano wa polisi mjini Dallas wiki iliyopita, yanaziumiza vichwa mamlaka husika hasa katika suala la umiliki wa silaha za moto.
Polisi nchini Marekani imesema sheria katika Jimbo la Texas inayoruhusu raia kutembea na silaha ni moja ya mambo yanayowapa ugumu kudhibiti matukio ya mauaji ya kutumia silaha ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
Mkuu wa Polisi katika mji wa Dallas, David Brown, ameyasema hayo kufuatia shambulio la kutumia silaha lililosababisha vifo vya polisi watano wiki aliyopita, ambalo limefanywa na mtu aliyekuwa akimiliki silaha.
Katika kuhakikisha Marekani inakabiliana na vitendo hivyo vya mauaji ya kutumia silaha, Rais Barack Obama alikutana na makundi mbalimbali mjini Washington, kuzungumzia njia tofauti za kuwapatia maofisa wa polisi mafunzo.
Na pia alitarajia kuutembelea mji wa Dallas kushiriki mazishi ya waliouawa katika shambulio hilo.