22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ubaguzi wa rangi ni saratani inayotafuna Marekani

Maandamano

KILICHOTOKEA Marekani siku nne zilizopita kimeichafua nchi hiyo inayojivunia kustaarabika kijamii kwani imeficha maradhi yanayoiumbua kwa vifo vya saratani ya ubaguzi wa rangi kwa yaliyotokea jijini Dallas.

Micah Johson aliyewaua polisi watano aliteka nyara ajenda ya waandamanaji waliokasirishwa na mauaji ya polisi weupe dhidi ya Wamarekani weusi, kama asingeuawa basi angeendeleza mikakati yake kwani upekuzi nyumbani kwake ulibainisha alikuwa anajiandaa kutengeneza mabomu.

Maandamano ya kupinga kuuawa kikatili kwa Wamarekani weusi wawili waliopigwa risasi na polisi Wazungu, Philando Castile (Minnesota) na Alton Sterling (Louisiana) yalimpa nafasi Micah kutimiza mauaji na mjini Tennesse polisi Mzungu aliuawa na Lakeem Scott, aliyedai kulipiza kisasi kwa mauaji ya polisi dhidi ya weusi nako Missouri askari mwingine aliuawa kwa kutunguliwa kisogoni na Georgia nako askari mwingine aliuawa alipoitika wito wa dharula alioupokea.

Kwa ujumla saratani ya ubaguzi imeibuka upya ikidhihirisha kuwa na mizizi mirefu kuliko inavyodhaniwa, ni mkanganyiko unaovuka viwango kwani Micah aliyewaua polisi Wazungu alikuwa mwanajeshi tangu mwaka 2009 hadi 2015 na amepigana vita nchini Afrighanistan.

Polisi walipojaribu kumshawishi ajisalimishe alidai kukasirishwa na mauaji ya polisi Wazungu dhidi ya Wamarekani weusi, tofauti na viwango vingine vya ubaguzi huu wa sasa unahusisha askari polisi Wazungu wenye silaha na mwanajeshi mstaafu mweusi mwenye ujuzi wa silaha hivyo kusababisha hatari kubwa ya mauaji.

Kilichotokea kimewalazimisha mahasimu wa kisiasa kuungana japo si kwa kupenda kukemea mauaji hayo ya kibaguzi, Obama amelaani vikali mauaji hayo akiwa kwenye kikao cha Nato nchini Poland naye Hillary Clinton mgombea urais wa chama cha Democrat amesikitishwa na vurumai, chuki na mauaji hayo akisema taifa linapaswa kuungana kutafuta suluhisho.

Donald Trump amesema kuwa mauaji hayo yametikisa mtima wa taifa kwamba kuna jukumu kubwa la kutafuta namna ya kuwahakikishia Wamarekani usalama wa maisha yao. Kama kinachotokea sasa kinakukanganya basi unapaswa kufahamu kuwa ni kilele cha mauaji ya hivi karibuni yaliyoanza mwaka 2014, mji wa Ferguson ulipozizima kwa vurumai baada ya mauaji ya Michael Brown akiwa mikononi mwa polisi.

Mwaka 2015 Fred Gray aliuawa huko Baltimore lakini sumu ya ubaguzi wa rangi haikuanza sasa nchini Marekani, kwani mwaka 1917 Wazungu waliwashambulia weusi na mauaji mengi kutokea wakipinga wasiajiriwe katika viwanda vya silaha. Mauaji ya vijana Wamarekani weusi miaka ya 1919, 1921, 1960 na 1964 yalisababisha Philadephia, Rochester na Harlem kukumbwa na vurumai kama ilivyotokea Dallas.

Polisi weupe wanalalamikiwa kwa kuwanyanyasa weusi.
Polisi weupe wanalalamikiwa kwa kuwanyanyasa weusi.

Marekani inahitaji kufuta doa la mauaji ya kibaguzi yaliyofikia pabaya vinginevyo maisha salama kwa raia wa rangi zote wa taifa hilo linaloundwa na jamii mbalimbali yatabaki kuwa hekaya tu.

Mamlaka nchini humo zinakosea kulazimisha waliohasimiana kuaminiana kwa shuruti, polisi wanadai weusi wawaamini kwani yanayotokea ni makosa binafsi ya baadhi ya askari wa jeshi hilo. Lakini katika hali ambayo polisi weupe hupelekwa kulinda vitongoji vya Weusi ni kutia petrol kwenye moto, ni kama askari hao wapo kwa ajili ya Weupe tu kwani hata wahamiaji wenye rangi mchanganyiko wakitoa taarifa za kufanyiwa uhalifu, huhamishwa kurudishwa walikotoka.

Ubaguzi umeongezeka zaidi ndani ya miaka nane ya utawala wa Obama anayebaguliwa hata na baadhi ya wanasiasa wenzake wabobevu wa Marekani, ni hujuma inayowafanya weusi wenzake wasimwelewe kwani wakilinganisha mauaji wanayofanyiwa sasa, kwao Bill Clinton ndiye aliyewajali zaidi kwamba ni ‘mweusi wa nafsi’ tofauti na rangi yake nyeupe ya ngozi.

Wamarekani wanapaswa kuutanzua mkanganyiko unaowakabili kwa kuangazia historia kwani jamii zao zote ni wahamiaji, waliowaondoa wenyeji wa asili waliokutwa na Christopher Columbus mwaka 1492 wengine wakafuatia kugombea maeneo baada ya ugunduzi wa Mtaliano Amerigo Vespucci aliyesababisha jina la Americus (America) lililotohoa jina lake kwa Kilatini. Lakini ndani ya taifa hilo kuna watu wenye asili ya sehemu mbalimbali ikiwemo kutoka Hispania, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Sweden na Afrika. Kwa hiyo tiba ya kung’oa mizizi ya hisia za ubaguzi inatakiwa iwe na dozi kubwa!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles