NA OSCAR ASSENGA, TANGA
UONGOZI wa klabu ya Coastal Union umeanza mchakato wa usajili wa wachezaji watakaong’ara kwenye kikosi hicho katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) itakayoanza kutimua vumbi mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Hemed Aurora, aliliambia MTANZANIA jana kuwa mchakato huo unafanywa na benchi la ufundi ambalo linaendelea na zoezi la kuangalia wachezaji wenye uwezo katika mazoezi yanayofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Alisema zoezi hilo ni hatua za mchujo wa awali unaofanyika ili kupata wachezaji mahiri watakaounda kikosi imara kitakachopambana katika harakati za kuiwezesha Coastal kurejea katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Katika hili niwatake wachezaji wajitokeze kwa wingi kwenye mchakato huo kwani ambao wataonekana kuwa na vipaji na uwezo mkubwa wataanza mazungumzo na uongozi ikiwemo kuanza kuhudumiwa na timu hiyo,” alisema.
Aurora alisema wachezaji ambao watafuzu majaribio watapata fursa ya kuonyesha viwango vyao katika michuano ya FDL ambayo Coastal imepangwa Kundi B na timu za JKT Mlale, Kimondo FC, KMC, Kurugenzi FC, Mbeya Worrios, Njombe Mji na Polisi Morogoro.
“Tunawahitaji vijana wenye uwezo wa kucheza soka wajitokeze kwa wingi kuhudhuria mazoezi yanayofanyika Uwanja wa Mkwakwani, kwani tumedhamiria kusajili wachezaji chipukizi walio na vipaji ili kuiwezesha timu kufikia malengo ya kurejea Ligi Kuu,” alisema.