BARCELONA, HISPANIA
KLABU ya Barcelona ya nchini Hispania imeanzisha kampeni mpya kwa mashabiki wote wa timu hiyo kwa ajili ya kumuunga mkono mshambuliaji wao, Lionel Messi, raia wa nchini Argentina.
Mchezaji huyo kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya kukwepa kodi, hivyo wiki iliyopita alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha kwenda jela miezi 21 pamoja na faini.
Hata hivyo, kwa sheria za mahakama za nchini Hispania, zinasema kwamba mtu yeyote ambaye atahukumiwa kwenda jela chini ya miaka miwili basi anaweza kuwa chini ya uangalizi ambao ni kifungo cha nje, hivyo mchezaji huyo anaweza kutumikia kifungo cha nje.
Uongozi wa mchezaji huyo umedai unatarajia kukata rufaa juu ya hukumu hiyo siku za hivi karibuni.
Kutokana na hali hiyo jina la Messi linaonekana kuchafuka hasa kutokana na jambo hilo pamoja na kushindwa kuisaidia timu yake ya Taifa kutwaa ubingwa wa michuano ya Copa America dhidi ya wapinzani wao Chile.
Klabu hiyo ya Barcelona imewataka mashabiki wote kumuunga mkono mchezaji huyo katika kipindi hiki kigumu ili ajisikie kuwa anathaminiwa.
Hivyo kampeni hiyo inajulikana kwa jina la #WeAreAllLeoMessi’ imeundwa na uongozi wa klabu hiyo kupitia mitandao ya kijamii.
Kila shabiki anatakiwa kuonesha sapoti yake kwa kuposti kampeni hiyo huku ikiwa na picha ya Messi ambayo imewekwa na klabu hiyo, hivyo shabiki anatakiwa kueleza hisia zake juu ya jambo hilo.
Hata hivyo, rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu, amekuwa wa kwanza kuonesha hisia zake kupitia kampeni hiyo, ametuma ujumbe huku akisema kwamba “Messi, kwa wale ambao watakushambulia ni sawa na wanaishambulia Barcelona na historia yake kwa ujumla, hivyo tutapambana kuhakikisha unakuwa huru. Kwa pamoja milele,” aliandika Bartomeu.