NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inadaiwa kumfungia kujihusisha na soka kwa kipindi cha mwaka mmoja Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya soka ya Yanga, Jerry Muro.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka ndani ya kamati hiyo, zinaeleza kuwa mbali na adhabu ya kufungiwa pia inadaiwa Muro ametakiwa kulipa faini ya shilingi milioni tatu.
Kikao cha kamati ya maadili kilikutana jana kujadili tuhuma zilizokuwa zikimkabili Muro kutokana na kupinga uamuzi wa TFF pamoja na kulishambulia shirikisho hilo katika vyombo vya habari.
Baada ya MTANZANIA kupata tetesi hizo, lilimtafuta Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, ili kuzungumzia suala hilo ambapo alisema bado hajapata taarifa rasmi juu ya uamuzi uliofikiwa na kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo.
Alisema hawezi kueleza lolote kuhusiana na jambo hilo kwa kuwa hajapata ufafanuzi wowote, hivyo atakuwa tayari kufanya hivyo baada ya kupata taarifa sahihi.
Awali, kabla ya kamati hiyo kukutana, TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa, ilimwandikia barua Muro Juni 29 mwaka huu ikimtaka msemaji huyo wa Yanga kwenda kujitetea kwenye kamati iliyopanga kukaa Julai 2, mwaka huu, kujibu tuhuma zinazomkabili.