NA WALTER MGULUCHUMA, Mpanda
CHAMA cha Wafugaji Tanzania (CCWT) mkoani Katavi, kinatarajia kuwapeleka Rwanda baadhi ya wanachama wao wakajifunze ufugaji bora.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa CCWT Mkoa wa Katavi, Mussa Kabushi alipozungumza kwenye kikao cha wafugaji mkoani hapa.
Kikao hicho kilihusisha pia wenyeviti wa halmashauri na madiwani wa halmashauri hizo.
“Tatizo linalowakabili wafugaji wengi hapa nchini ni ukosefu wa elimu ya ufugaji bora wa kisasa. Kwa kulitambua hilo, sasa tumeamua kuwapeleka baadhi ya wanachama wetu Rwanda wakajifunze ufugaji bora wa kisasa.
“Kilio kikubwa kwa wafugaji wa Mkoa wa Katavi ni kutotengewa maeneo ya kufugia na hali hii imekuwa ikiwafanya baadhi ya wafugaji kufugia kwenye maeneo yasiyostahili na kusababisha migogoro isyokuwa na maana.
“Kwa hiyo tunaiomba Serikali ya mkoa wetu, ifanye kila linalowezekana tupate maeneo hayo kwa ajili ya kuimarisha ufugaji wetu,” alisema Kabushi.
Naye Meya wa Manispaa ya Mpanda, Willy Mbogo, aliviomba vijiji vyenye ardhi kubwa vitenge maeneo ya wafugaji kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Raphael Kalinga, alisema Mkoa wa Katavi unakabiliwa na tatizo la wingi wa mifugo kwa kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakiingia mkoani humo kutoka mikoa mingine nchini.
Aliwataka wafugaji waache tabia ya kusafirisha mifugo na kuipeleka katika maeneo yasiyostahili.