NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Simba, Mcameroon Joseph Omog, leo anaanza rasmi safari yake ya kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuanza kibarua cha kukisuka upya kikosi hicho ili kurudisha heshima ya ubingwa kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Ujio wa Omog ndani ya kikosi cha Simba, umeongeza matumaini ya kufanya vizuri kwa kikosi hicho msimu ujao kwani mashabiki wamechoka kelele za mahasimu wao Yanga wanaowaita wa ‘mchangani’.
Kutokana na kukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo, Simba sasa wamejipanga kuhakikisha msimu ujao unakuwa wa mafanikio kutokana na rekodi ya kocha huyo mpya aliyoiweka wakati akiifundisha Azam FC.
Mahasimu wao Yanga wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo jambo linalowapa jeuri Simba kutokana na wao kushiriki michuano ya kimataifa huku wapinzani wao wakishindwa kufanya hivyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, Omog alielezea nia yake ya kutaka kujenga kikosi imara kitakachotwaa ubingwa msimu ujao ili kufuta machungu ya mashabiki wa Simba.
“Kilichonileta Simba ni kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwa ushirikiano mkubwa kati ya benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki.
“Nafahamu kuna changamoto ya timu kukosa ubingwa kwa misimu kadhaa lakini tunaweza kufikia malengo hayo endapo tu umoja utakuwepo ndani ya klabu,” alisema.
Alisema hana shaka na wachezaji waliobaki ndani ya kikosi cha Simba na wale waliosajiliwa kwa msimu ujao huku akieleza kuwa kazi kubwa iliyobaki ni kuifanya timu hiyo kuwa bora zaidi kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.