SANTIAGO, CHILE
NYOTA wa timu ya taifa ya Chile na klabu ya Arsenal, Alexis Sanchez, amekosa sherehe za ubingwa wa michuano ya Copa America kutokana na kuwa majeruhi.
Mchezaji huyo alipata majeruhi katika mchezo wa fainali ya Copa America dhidi ya Argentina, huku timu yake ikifanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.
Sanchez ambaye aliibuka mchezaji bora wa michuano hiyo kwa sasa anasumbuliwa na tatizo la kifundo cha mguu hivyo alishindwa kuungana na wachezaji wa timu hiyo ya taifa katika sherehe za ubingwa huo.
Mchezaji huyo alituma video yake kwa mashabiki wa timu hiyo ya taifa kupitia akaunti yake ya Instagram, ambapo aliwatoa wasiwasi kwa kuwaambia anaendelea vizuri japokuwa ameshindwa kuungana na wenzake.
“Najua mashabiki wa Chile walitamani kuniona katika sherehe za ubingwa wa Copa America, lakini nimeshindwa kutokana na hali yangu ya mguu, lakini nashukuru ninaendelea vizuri na muda mfupi ujao nitarudi uwanjani,” alisema Sanchez.
Hata hivyo, mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Eduardo Vargas, aliwafurahisha mashabiki ambao walijitokeza kwenye sherehe hizo ambazo zilifanyika kwenye uwanja wa Santiago Estadio Nacional, baada ya kuwaambia kwamba wapinzani wao ni kama watoto kwao.
“Hii ni mara ya pili kukutana na Argentina kwenye fainali ya michuano ya Copa America na zote tunafanikiwa kushinda, hivyo ni wazi kwamba Argentina kwetu ni kama watoto, wanajitahidi kufika fainali lakini kazi yetu ni kuwatoa na kuchukua ubingwa,” alisema Vargas.