NA JOCELYN JAMES,
MKALI wa muziki wa Bongo Fleva aliyewahi kutamba na wimbo wa ‘Chura’ kisha ukafungiwa kutokana na kukiuka maadili ya Mtanzania, Snura Mushi ‘Snura Majanga’, amedai kushangazwa na Bodi iliyokaa na kutopitisha muswada (script) mpya ya marudio ya video yake hiyo wakati anaamini ameikamilisha kama ilivyotakiwa.
Video ya ‘Chura’ ilizuiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na ilimwagiza Snura aiwasilishe ‘script’ mpya ambayo hata hivyo baada ya kufanya hivyo nayo imekataliwa kwa madai kwamba inaonekana kuendana na iliyofungiwa.
Snura aliliambia MTANZANIA kwamba ameshangazwa na uamuzi huo kwa kuwa ameshabadili mfumo wote wa uchezaji ulioonekana kutokuwa na maadili kwa jamii na ameweka uchezaji mpya ambao utamwonyesha yeye akiwa na msichana mmoja anayefikisha ujumbe uliokusudiwa kufika.
“Kiukweli nashangaa uamuzi huo na ni kwanini hawajakubali ‘script’ ya wimbo wangu wakati nimeshabadilisha mfumo mzima wa uchezaji na baadhi ya vipande visivyotakiwa wakiwemo wale wasichana wote nimewatoa, nashindwa kuelewa kwanini imekuwa hivyo,” alieleza Snura.
Hata hivyo, Snura aliendelea kuwataka mashabiki wake wasiendelee kusubiri video mpya ya wimbo huo ambayo anaendelea kubadilisha ‘script’ yake hadi itakapokubaliwa na mamlaka zinazohusika.