Na Gabriel Mushi, Dar es Salaam
CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kinatarajia kuufanyia utafiti ugonjwa wa ajabu ulioibuka mkoani Dodoma kupata suluhisho la ugonjwa huo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya, wakati akifunga mkutano wa nne wa wataalamu wa sekta ya afya ulioandaliwa na MUHAS Dar es Salaam.
Alisema chuo hicho kimekuwa kikifanya utafiti mbalimbali unaoisaidia serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya, hivyo ni jukumu lake kuufanyia utafiti ugonjwa huo wa ajabu ulioibuka katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.
“Tumepanga kuisaidia serikali kuufanyia utafiti ugonjwa huo kwa sababu umekuwa ukisababisha mtafaruku ndani ya jamii bila kufahamu chanzo chake halisi na hata suluhisho lake… Muhas tutaanza jukumu hilo hivi karibuni.
“Taifa hili bado linakabiliwa na matatizo ya afya na bila sayansi huwezi kuelewa mbinu za kutatua matatizo yanayotukabili, hivyo tutaendelea kufanya utafiti kutatuta changamoto zinazoikabili jamii yetu,” alisema.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, John Michael, alisema tayari sampuli za ugonjwa huo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali kwa uchunguzi.
“Uchunguzi wa kina utakaofanywa na Muhas utaisaidia serikali kupata suluhisho lake kwa sababu sasa uchunguzi wa awali umeonyesha ugonjwa huo umesababishwa na sumu kuvu ambayo ni kemikali inayopatikana katika nafaka,”alisema.
Ugonjwa huo wa ajabu uliripotiwa kuibuka Juni 17 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu saba na hadi sasa wengine 32 wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa na ya Rufaa Dodoma.