LONDON, ENGLAND
KOCHA wa klabu ya Arsenal raia wa Ufaransa, Arsene Wenger, amedai kwamba kiungo wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Paul Pogba, hafai kuwa kiongozi ndani ya kikosi hicho.
Wenger amesema timu hiyo ni kubwa katika ulimwengu wa soka, hivyo anatakiwa mchezaji ambaye ana uzoefu mkubwa kwa ajili ya kuwaongoza wenzake katika michuano mbalimbali ili kuleta heshima ya taifa.
Amedai kwamba, umri wa Pogba ni mdogo hivyo hawezi kuongoza timu kubwa kama Ufaransa japokuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza soka.
“Tunatarajia makubwa kutoka kwa Pogba katika soka la sasa hasa katika usajili kutokana na uwezo wake, lakini kutokana na umri wake naweza kusema kwamba mchezaji huyo hawezi kuwa kiongozi wa timu ya Taifa kama Ufaransa, ana umri wa miaka 23, naweza kusema ni mdogo anatakiwa kupatikana mchezaji ambaye ana uzoefu mkubwa.
“Wakati Michel Platini na Zinedine Zidane, wanaitumikia timu ya Taifa walikuwa kwenye kiwango kizuri lakini hawakuwa viongozi wakiwa na umri mdogo japokuwa walikuwa na kiwango kizuri, hivyo Pogba anatakiwa kupewa muda, labda akifikisha miaka 26 itakuwa sawa lakini si kwa miaka hii 23,” alisema Wenger.