27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yacharuka sakata la Kessy

kessy
kessy

NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM

IKIWA imebaki siku moja kabla ya kuchezwa mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), klabu ya Simba imeibuka na kudai haijapokea barua kutoka kwa mahasimu wao ya kuomba ridhaa ya kumtumia beki Hassan Ramadhani ‘Kessy’.

Yanga ilishindwa kumtumia Kessy katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi A dhidi Mo Bejaia ya Algeria kutokana na agizo la Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kutaka barua rasmi kutoka Simba inayothibitisha kuwa wamemalizana na beki huyo.

Wawakilishi hao pekee wa Tanzania walitaka kumtumia Kessy aliyesajiliwa mwishoni mwa msimu uliopita kutokana na beki tegemeo, Juma Abdul kuwa majeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara, Yanga hawawezi kumtumia Kessy hadi watakapoamua kutumia uungwana wa kuandika barua.

“Simba hatujapokea barua yoyote, wanachofanya Yanga ni kutaka kuichafua klabu yetu kwa wapenzi na mashabiki wa soka, waache kudanganya umma, msimamo wetu katika suala la Kessy utategemeana na uungwana watakaofanya watani wetu,” alisema.

Manara alitoa mfano wa mwaka 1998 wakati Simba ilipoiazima wachezaji watatu wa Yanga ili wacheze katika hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Afrika amabo ni Shaban Ramadhani, Monja Liseki na Alphonce Modest na kuhoji watashindwaje kumruhusu mchezaji ambaye wamemsajili.

“Pamoja na maneno yao ya kuudhi Simba ni waungwana hivyo wasitumie ukimya wetu kuwapotosha wanachama na mashabiki wetu kwa madai tumekataa kujibu barua ya kumtumia Kessy,” alisema Manara.

Aliongeza kuwa hakuna barua yoyote wala mazungumzo yaliyofanyika baina yao walau Yanga kuomba baraka hata kwa mdomo na kwamba Simba haina tatizo katika kuruhusu matakwa  binafsi ya mchezaji na kwamba kila mtu analifahamu hilo.

Aidha, Manara aliwataka Yanga kutoruhusu mashabiki wao kutumia majukwaa ya upande wa Simba katika mchezo wa kesho dhidi ya TP Mazembe kama ilivyodaiwa na Mkuu wa Idara ya habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro.

“Kauli hiyo ina nia ya kuchochea vurugu katika mchezo huo na wote tunafahamu athari zake michezoni, tunawashauri Yanga wasijaribu kuruhusu mashabiki wao kukaa kwenye majukwaa ya Simba ili kuongeza amani na kukwepa matatizo yanayoweza kujitokeza,” alisema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe, alisema hawaweza kumruhusu Kessy kuichezea Yanga kabla ya kufika Juni 30, mwaka huu.

Upo uwezekano mkubwa wa Yanga kumtumia Abdul kama beki wa kulia katika mchezo dhidi ya TP Mazembe baada ya afya yake kuimarika na kuanza mazoezi tangu wiki iliyopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles