Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS John Magufuli ametumbua majipu saba, yakiwamo ya wastaafu hewa, miamala ya simu na riba kwa mabenki, huku akisema kuwa Serikali yake haiko tayari kuwavumilia wachimbaji wa madini wanaoliingizia taifa hasara.
Mkuu huyo wa nchi, alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alisema hivi sasa yupo katika mapambano ya kukomesha watumishi hewa, na hadi kufikia jana wamefikia 12,446 na kwamba ana uhakika bado wanaendelea kuwapo na wengine watapatikana.
WASTAAFU HEWA
Rai Magufuli alisema kutokana na hali hiyo, alijiuliza kuhusu wastaafu hewa ambao imebanika wapo 2,800 na wamelipwa Sh bilioni 7 na Benki ya NMB.
“Mpaka sasa mafao ya kustaafu hewa (pensheni) kuna watu 2,800 wamelipwa Sh bilioni 7 na Benki ya NMB, na nimeshaagiza warudishe fedha hizo. Nilitoa agizo ajira kwa sasa zisimame kwa mwezi mmoja au hata miwili ili tuweze kuondoa tatizo hilo, Serikali inalipa mishahara kila mwezi Sh bilioni 577,” alisema.
Rais Magufuli alisema hana nia mbaya na wafanyakazi bali anachotaka ni kumaliza tatizo lililopo, kwani wafanyakazi hewa ni ugonjwa wa kansa.
AKAUNTI MFU
Pamoja na hali hiyo, Rais Magufuli aliitaka BoT izitazame akaunti mfu (Dormant Account), na kwamba anawaacha wasubiri aone kama wataziangalia.
“Hazina na BoT Dormant Account naomba mzitazame, kwani nyie mnazifahamu, nawaacha nione kama mtaziangalia. Mimi nafahamu kuna akaunti moja ina shilingi bilioni 32,” alisema.
KODI YA MADINI
Rais Magufuli pia aliyashukia makampuni ya madini nchini yanayokwepa kodi na kudai yanajiendesha kwa hasara, na kueleza wazi kuwa Serikali yake iko tayari kubaki na madini ardhini kuliko kuwaachia wachimbaji hao.
Alisema wote wanaoona hawapati faida katika shughuli zao, ni bora wakaondoka na kuyaacha madini hayo ili vizazi vijavyo viweze kunufaika.
“Haikubaliki wewe kila mwaka unasema umepata hasara tu, mwaka wa kwanza, wa pili wa tatu wa kumi unapata hasara tu, si uondoke, hivyo ni visingizio tu, bora tubaki na madini yetu miaka 1,000 watachimba watakaokuja sisi tukiwa tumeoza. Wanadai wanapata hasara, lakini wana akaunti sehemu nyingine,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, aliitaka BoT kusimamia kikamilifu mapato ya kampuni za madini.
MIAMALA YA SIMU
Mbali na hilo, pia amewataka BoT wakishirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) pamoja na Hazina, kuhakikisha Serikali inapata mapato kutokana na miamala ya simu.
Alisema pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na BoT, lakini wanapaswa kuhakikisha wanalinda usalama na ubora wa huduma za fedha, ikiwamo matumizi ya fedha kwa simu ili Serikali ipate mapato.
Rais Magufuli alisema anazo taarifa kuwa Machi mwaka huu kuna miamala (trasanction) ya simu iliyofanyika yenye thamani ya Sh trilioni 5.5.
Kutokana na hali hiyo, alihoji endapo Serikali ilinufaika na miamala hiyo.
“BoT ijipange kutazama suala hilo, mshirikiane na TCRA na Hazina kuhakikisha Serikali inapata mapato kutokana na miamala ya simu,” alisema.
RIBA KWA MABENKI
Alisema BoT inapaswa kushughulikia suala la riba ipasavyo kwa kile alichosema taasisi nyingi zilizo na ujasiri wa kukopa zimeishia kufilisika kutokana na riba kubwa katika mabenki.
Alieleza kuwa benki na taasisi ambazo zinakiuka masharti ya BoT zichukuliwe hatua hata kama ni za Serikali.
Alisema benki ya Twiga Bancorp, imekuwa ikijiendesha kihasara, huku akimtaka Gavana Benno Ndulu, kuifuta kwani imekuwa hata ikivunja sheria.
Rais Magufuli ameiagiza BoT kuchukua hatua mara moja dhidi ya benki ambazo hazizalishi faida zikiwemo za Serikali
“Unakwenda benki unakuta kuna negative ya shilingi bilioni 18, mimi nasema katika utawala wangu sitabembeleza benki isiyofanya vizuri hata kama ni ya Serikali. Kuna benki moja inapambwa sana na CCM (hajaitaja jina) lakini mmh,” alisema Rais Magufuli huku akicheka.
Akieleza changamoto zilizopo alisema kuwa ni idadi ndogo ya Watanzania wanaonufaika na huduma za benki, hususani waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo kusababisha wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa.
MADUKA YA FEDHA
Akizungumzia kuhusu usimamizi wa vyombo vingine vya fedha, alisema ni vyema BoT ikasimamia kwa makini maduka ya kuuza fedha za kigeni ili kujua uhalali wake na yasitumike kuingiza fedha za dawa za kulevya au yasiwe sehemu ya kutoroshea fedha.
“Mnatakiwa kulinda thamani ya shilingi, zipo njia mnaweza kuzitumia kudhibiti mporomoko na matumizi ya fedha za kigeni, naomba mshirikiane na vyombo vingine ili suala hilo lidhibitiwe, mtaweza kuzuia utakatishaji wa fedha na kudhibiti wauzaji wa unga,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu kushuka kwa mfumuko wa bei, alisema mfumuko huo usishuke kwenye makaratasi bali unapaswa kuonekana wazi kwa wananchi, kwa kuwa bado hawajaona kama kweli umepungua.
“Mmeniambia kwamba mfumuko wa bei umeshuka kutokana na jitihada zenu kutoka asilimia 30 hadi kufikia 5.2. Je, umefika kwa wananchi au unaishia kwenye makaratasi tu? Je, bidhaa zilizotumiwa miaka ya 90 na sasa ni sawa?” alihoji.
Pamoja na hali hiyo, ameitaka BoT kuhakikisha ushukaji wa mfumuko wa bei uliotoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 5.1 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, unaonyesha matokeo katika nafuu ya maisha ya Watanzania.
PROFESA NDULU
Awali akifungua sherehe hizo, Gavana wa BoT, Profesa Ndulu, alisema benki hiyo imepiga hatua kubwa kwa kuweza kupunguza mfumuko wa bei. Mwaka 1995 ulikuwa asilimia 28 na kwamba hadi kufikia Mei, mwaka huu umefikia asilimia 5.2.
Alisema BoT kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika dhana ya elimu bure ili ifanikiwe, wanachangia Sh bilioni 4 kwa ajili ya kununua madawati.
“Mheshimiwa Rais, leo tutakukabidhi mfano wa hundi wa Sh bilioni 4 kwa ajili ya kutatua changamoto ya uhaba wa madawati, fedha hizi zinatokana na ubanaji wa matumizi. Ombi letu fedha hizi zielekezwe mikoa yenye matawi ya BoT ambayo ni Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza, Zanzibar na Mtwara,” alisema Prof. Ndulu.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile, alisema watazidi kuimarisha sekta ya fedha ili kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi.
SARAFU YA SH 50,000
Pia, Rais Magufuli alizindua sarafu ya Sh 50,000 ambayo hata hivyo haitaingia kwenye mzunguko wa fedha, ikibaki kama kumbukumbu ya miaka 50 ya BoT.
Sarafu hiyo ina uzito wa gramu 29, umbo la mzunguko, upande wa nyuma ina nembo ya BoT na mbele ikionyesha benki hiyo, huku ikiwa na madini ya fedha kwa asilimia 99.
MAKONDA
Awali akizungumza kwenye sherehe hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema katika mkoa wake imefikia hatua Sh bilioni 3.6 zinalipwa kwa wafanyakazi hewa.
Pamoja na hilo, alisema Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, amekuwa msaada mkubwa, kwani amesadia kufunga akaunti za watumishi hewa, huku wengine wakikamatwa na vyombo vya usalama wakati wakijaribu kutoa fedha hizo.
Kuhusu uhaba wa madawati, alisema Mkoa wa Dar es Salaam, una wanafunzi 480,000, madawati yanayotakiwa ni 66,134 kwa shule za msingi 34,000 shule za sekondari.
“Mheshimiwa Rais, mkoa wangu wa Dar es Salaam unachangia kwenye pato la taifa kwa asilimia 60, lakini tuna uhaba wa madawati 66,134, kwani tuna wanafunzi 480,000. Tuna upungufu wa vyumba vya madarasa 7,514 kwa shule za msingi na 803 kwa shule za sekondari,” alisema Makonda.
Akizungumzia kuhusu kuwaondoa ombaomba, alisema kutokana na utafiti walioufanya, wamebaini kwamba wazazi wamekuwa wakiwatumia watoto wadogo kuomba mitaani.
“Tumewakamata ombaomba 135, kati ya hao 65 ni watoto. Hivyo kwa sasa tunafanya utaratibu ili wote waende shule wakasome hapahapa.”
Sherehe hizo zilizohudhuriwa na magavana na manaibu gavana kutoka nchi 18, ziliambatana na uzinduzi wa vitabu viwili; kimoja kikielezea historia ya BoT na mtazamo wa miaka ijayo na kingine kuhusu changamoto za Tanzania katika kufikia uchumi wa juu.