30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Si kila uhalifu ni ugaidi              

nchemba1UGAIDI, ugaidi, ugaidi! Ugaidi unaikosesha raha dunia. Sehemu nyingine za dunia ugaidi umewafanya watu walale usiku kucha macho yakiwa wazi huku wengine wakizikimbia nyumba zao za kifahari.

Je ugaidi huu unaomtesa kila mtu bila kuangalia kama ni tajiri au masikini, msomi kwa asiyesoma, mweusi kwa mweupe ni mdudu gani? Je jamaa huyu ugaidi alianza vipi katika sura ya  dunia?

Ni vigumu kupata tafsiri halisi ya neno ugaidi kwa maana ya kwamba uhalifu  unaweza  kutathiminiwa  kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi kulingana na matakwa ya nchi husika.  Mtu anaweza kufanya tukio fulani katika China akaitwa gaidi lakini tukio lile likafanywa na mwingine huko Angola akaonekana mkombozi.

Tafsiri tata ya ugaidi ndiyo ilipelekea  Marekani kumuita  Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela  gaidi kutokana na harakati zake za kudai uhuru,  wakati kiongozi huyo  kwa upande wa Afrika Kusini na bara la Afrika kwa ujumla akichukuliwa  mkombozi.

Mbali na tafsiri ya ugaidi kuleta mkanganyiko lakini kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili la mwaka 2002 inaelezea kuwa ugaidi ni “vitendo vya kutisha; kutumia nguvu; mauaji na mashambulizi yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo fulani ya kisiasa.”

Umoja wa mataifa umetafsiri neno ugaidi kuwa ni “vitendo vya kijinai ambavyo hukusudia kuchochea vitisho katika umma, makundi ya watu au watu fulani kwa malengo ya kutimiza siasa. Ni katika misingi ya kisiasa, kifalsafa, kiitikadi, ubaguzi wa kikabila, ubaguzi wa kidini au hali yoyote inayoweza kutumika kwa nia ya kutambulisha kundi hilo la ugaidi.”

Na kwa upande wake Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) katika utafiti wake wa mwaka 2002 linatafsiri neno ugaidi kuwa ni “vitendo vinavyokiuka sheria kwa kushurutisha au kutumia nguvu sana dhidi ya watu au mali ili kutisha serikali au raia kwa malengo ya kutimiza matakwa ya kisiasa au kijamii.”

Hata hivyo kulingana na ugaidi kuwa tishio katika sayari ya dunia, inaonekana binadamu wameathirika kisaikolojia na hivyo kushindwa kutofautisha aina za uhalifu kulingana na matukio yanayotokea na hivyo kupelekea kila tukio lenye kumwaga damu kuitwa ugaidi.

Ukweli ni kwamba ugaidi ni aina mojawapo ya uhalifu lakini si kila uhalifu ni ugaidi.  Uwezekano ni asilimia 100 kwamba ndani ya ugaidi vimelea vyote ni uhalifu lakini uwezekano unakuwa mdogo kwamba katika  kila uhalifu lazima ukute vimelea vya ugaidi.

Ni ukweli usiopingika kwamba kumwaga damu kumekuwepo tangu binadamu wa kwanza walipoumbwa kiasi kwamba enzi hizo msamiati wa ugaidi haukuwepo. Kwenye Biblia katika kitabu cha Mwanzo ukrasa wa 4 kitabu ambacho kimsingi hata ndugu zetu Waislamu wanakitambua, unakutana na mauaji ya Kaini kumuua nduguye Abeli kutokana na wivu.

Ni mara ngapi watanzania waishio mikoa ya mipakani kama Kigoma, Kagera, Rukwa na hata Geita wamekuwa wakikumbana na dhahama ya kupigwa risasi ovyo kutokana na tishio la ujambazi? Je uhalifu wa namna hii ambao umekuwepo kwa muda mrefu nao uitwe ugaidi?

Nje ya mikasa ya ujambazi wa kutumia silaha ni mara ngapi wananchi kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitekwa ili kuchunwa ngozi mfano Mbeya kutokana na fikra mfu za ushirikiano kama ilivyotokea Bukoba, wananchi ambapo waliwahi kukosa usingizi kwa kuhofia kutekwa ili kukatwa koromeo? Je uhalifu wa namna hii nao ni ugaidi?

Ni binadamu yupi katika taifa letu ambaye hajawahi kusikia au kuona watu wenye  ulemavu wa ngozi wanavyochinjwa kama wanyama katika taifa lao kutokana na mawazo ya kipumbavu ya kishirikina kwamba ngozi za viumbe hawa zinaleta utajiri? Je uhalifu huu usio na chembe ya huruma nao ni ugaidi?

Je ni mtanzania yupi ambaye hajui kuwa bibi zetu vikongwe hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Shinyanga ikiongoza kwamba  kutokana na macho yao kuwa mekundu kutokana na  matumizi ya kuni na umri  mrefu  wamekuwa wakikatwa mapanga na jamaa zao wa karibu ? Je na uhalifu huu ni ugaidi?

Ni mara ngapi katika taifa letu, kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia mauaji ya kutisha yanayotokana na kulipizana visasi kutokana na migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji? Je mauaji haya nayo ni ugaidi?

Je ni mara ngapi kwa muda mrefu pamekuwepo na mauaji mengi  yanayotokana na wivu wa kimapenzi ambapo mmojawapo wa wanandoa anaweza kumuua mwenza kama si kuteketeza familia nzima. La kujiuliza  mauaji hayo nayo  ni ugaidi?

Hivi yupo mwananchi ambaye hajawahi kuona au kusikia kwamba watu fulani wameuana kutokana na kudhulumiana mali ambapo wauaji wanaweza kukodiwa kutoka mbali ili kutimiza lengo? Je mazingira ya namna hii nayo ni ugaidi?

Je kwenye dini zetu kuu kwa maana ya dini ya Kikristo na Kiislamu ambapo pamekuwa pakijitokeza migogoro inayotokana na kugombania madaraka  waumini wasio waungwana hawawezi kudai haki yao kwa kufanya mauaji? Ikitokea mauaji haya tuyabatize jina ugaidi?

Katika  dunia ya sasa  ambapo ugaidi ndiyo habari ya mjini, watanzania na wananchi kwa ujumla hatuna budi kuwa macho na dhana ya neno hili kwa maana watu wasiotutakia mema wanaweza kutoa tafsiri hasi kwa matakwa binafsi ili kutujengea chuki na uadui.

Watanzania kwa umoja wetu bila kujali dini zetu na makabila yetu hatuna budi kutambua kuwa ugaidi si misingi ya dini fulani bali ni watu wachache ambao hujivika mwavuli wa dini kutekeleza hujuma ili kutimiza kiu yao.

Ndugu Joseph Kony  wa Uganda anayemwaga damu ya Waganda na nchi jirani kwa kutumia Biblia akijidai anawatetea watu, uhalifu wake wa kujificha kwenye ukristo hauwezi kuchukuliwa kuwa wakristo wote dunia nzima hufanya hivyo.

Tunaposikia kuwa Boko Haram huko Nigeria wakimwaga damu ya watu wasio na hatia huku wakitumia Kurani tukufu kujifanya wanatetea wanyonge, uhalifu wao wa kujificha kwenye Uislamu hauwezi kuchukuliwa waislamu wote dunia nzima hufanya hivyo.

Hata hivyo uhalifu wa kumwaga damu isiyo na hatia iwe kuua kwa  misingi ya ugaidi, ujambazi, ushirikina, wivu wa mapenzi au kulipizana visasi, hakika haukubaliki hata kidogo. Ni wajibu wa kila mwananchi kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuzika mauaji haya ili yabaki kwenye jumba la makumbusho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles