32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa kupewa chakula Muhimbili

mtz1VERONICA ROMWALD NA SECILIA ALEX (A3), DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imeanzisha utaratibu mpya wa kutoa chakula kwa wagonjwa kwa malipo ya Sh 30,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha,  alisema  mabadiliko hayo yataanza Julai Mosi, mwaka huu.

Aligaesha alisema kuwa hospitali itabeba jukumu hilo kutokana na malipo hayo na kwamba mgonjwa atapatiwa huduma hiyo kwa milo yote mitatu kwa siku.

“Pindi utakapoanza utaratibu huu Julai Mosi mwaka huu, katika wodi zote wauguzi watakuwa pia na kazi ya kumuuliza mgonjwa aeleze aina ya chakula anachopenda.

“Na hii itakuwa kuanzia kifungua kinywa, chakula cha mchana hadi usiku, tena chakula kitakuwa ni cha uhakika,” alisema.

Alisema katika utaratibu huo mpya, watatoza Sh 50,000 pindi watakapompokea mgonjwa, ambazo Sh 10,000 zitakuwa ni kwa ajili ya kitanda, Sh 10,000 ya kumuona daktari na Sh 30,000 itakuwa ni chakula kwa siku zote atakazokuwepo mgonjwa hospitali.

Aligaesha alisema kutokana na mipango hiyo mipya, hospitali hiyo inakadiria kwamba mgonjwa atakayepokewa atakaa wodini kwa muda wa siku tano.

“Awali mgonjwa alilipia Sh 20,000 ambazo Sh 10,000 ilikuwa ni kwa ajili ya kulazwa na Sh 10,000 iliyobaki kumuona daktari. Hivyo sasa atalazimika kulipia Sh 50,000, kwa ajili ya kupata huduma ya kulazwa, kumuona daktari na chakula,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, wamejipanga huduma zote zikiwemo za vipimo vya MRI na CT Scan ambavyo kwa sasa hupatiwa wakati wote hospitalini hapo kukamilishwa kwa kipindi kifupi.

Aligaesha alisema hospitali hiyo imeingia ubia na mzabuni Usambara Groceries na kwamba inaamini hatua hiyo ya kutoa huduma ya chakula itasaidia kuwapunguzia mzigo wa gharama ndugu wa wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo.

Alisema wamejipanga kutoa huduma bora ya chakula ambapo kwa wiki wagonjwa watakula ugali mara tano, wali mara tatu, pilau mara mbili na viazi mara tatu.

“Kabla hatujaleta huduma hii tulifanya tathmini, tukabaini ndugu wamekuwa wakiingia gharama kubwa kuwaletea chakula wagonjwa wao, kwa siku mtu mmoja hutumia nauli kati ya Sh 6,000 hadi 10,000 na hiyo hutegemeana na mahali anapotoka, bila kuweka gharama za chakula anachokiandaa kumletea mgonjwa wake,” alisema.

Alisema pia ndugu hao walilazimika kuacha shughuli zao za uzalishaji ili kuwapelekea chakula wagonjwa wao mara tatu kwa siku.

“Wanaingia gharama kubwa, tumetafuta mzabuni kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula ili hospitali tujikite katika huduma za msingi ambazo ni ushauri, uchunguzi na matibabu,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya ndugu ambao hushindwa kuwapelekea chakula wagonjwa wao, na wao kulazimika kuwapatia kile ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya wagonjwa wanaotoka mikoani na wale wasiokuwa na ndugu.

“Kumekuwa na ongezeko la msongamano wa watu ndani ya hospitali kuanzia saa 12 asubuhi hadi jioni. Hii inaleta changamoto ya kiusalama, kuna wizi wa vifaa vya magari.

“Lakini pia ule muda wa saa sita hadi nane ambao ndugu huja kuona wagonjwa huwa majopo mbalimbali ya wataalamu yanaendelea na raundi za kuhudumia wagonjwa wodini, hali hiyo wakati mwingine husababisha mgonjwa kutopata huduma stahiki,” alisema.

Alisema wamefuta muda huo na kwamba muda wa kuona wagonjwa ni saa 12 hadi moja asubuhi au saa 10 hadi 12 jioni, na ndugu watakwenda bila kubeba chakula labda matunda au maji.

Wakati huohuo, Kaimu Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema hospitali hiyo haitozi gharama za dawa za ARVS kama ilivyoripotiwa na chombo kimoja cha habari (si MTANZANIA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles