MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive (Jiji) jijini Dar es Salaam, imewahukumu watu wanane kulipa faini ya Sh 400,000 baada ya kupatikana na kosa la kuombaomba na uzururaji katika maeneo ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa hao walitiwa hatiani baada ya kukiri kosa la uzururaji na kuombaomba mitaani na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Jiji, Tarisila Kisoka, aliwahukumu kila mmoja kwenda jela miaka minne au kulipa faini Sh 50,000.
Washtakiwa hao ambao walilipa faini na kuachiwa huru ni Shukrani Dickson (28), Abdallah Hamis Ngwele (28), Shukuru Iddy (27), Haruni Salum (24), Issa Maganga (34), Saimon Malinya (45), John Mbonde (30) na Christina Pima (58).
Awali, mwendesha mashtaka, Ramadhani Kalinga, alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo wakiwa katika maeneo la Wilaya ya Temeke, mnamo Juni 16, mwaka huu.
Mwendesha mashtaka, Kalinga alidai kuwa washtakiwa walikamatwa na Ofisa wa Jiji aliyemtaja kwa jina la Hilda Kifanga.
Wakati huohuo washtakiwa wengine 12 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuzurura na kuombaomba kesi yao imeahirishwa hadi Juni 28, mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo.