Na Mwandishi Wetu, DODOMA
SERIKALI za Tanzania na Sweden zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa miaka minne kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2019 utakaojikita kuimarisha uchumi wa nchi na maendeleo ya watu katika nyanja mbalimbali yakiwamo elimu, utafiti, nishati jadidifu na kupambana na umasikini.
Makubaliano hayo yalifikiwa mjini hapa jana, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Ulrika Modeer.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Dk. Likwelile, alisema kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2019, Serikali ya Sweden itatoa ruzuku ya fedha za Kiswidi, SEK 5.5 Biln, sawa na Sh trilioni 1.42.
Alisema kutiwa saini kwa mkataba wa ushirikiano huo kunatokana na kusaini mikataba ya fedha.
Fedha hizo zitaelekezwa katika miradi kadhaa ikiwamo kusaidia elimu, maendeleo ya jamii-TASAF, utafiti, nishati, demokrasia, haki za binadamu na sekta binafsi.
“Ushirikiano huu umelenga kusaidia kujenga mazingira ya maendeleo endelevu na kuwapatia Watanzania maskini fursa za kujikwamua katika umaskini kwa kujipatia ajira na a kuanzisha biashara za kujipatia kipato ambako vikundi vinavyolengwa zaidi ni wanawake, watoto na vijana,” alisema Dk. Likwelile.