ORLANDO, FLORIDA
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Brazil, Philippe Coutinho, amempagawisha kocha wake, Carlos Dunga kwa kuifungia timu yake mabao matatu katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Haiti, kwenye michuano ya Copa America.
Mchezaji huyo ameifikia historia ya miaka 10 kwa mchezaji wa timu hiyo kufunga mabao matatu kwenye michuano ya Copa America, ambapo mara ya mwisho yalifungwa na Robson de Souza ‘Robinho’ mwaka 2006.
Katika ushindi huo wa jana, Dunga amesema amefurahishwa na wachezaji wake kuonesha uwezo huo lakini amempongeza Coutinho kwa kufunga mabao matatu.
“Tulianza vibaya kwa mchezo wa kwanza katika michuano hii ambapo tulitoka bila kufungana na Ecuador, lakini sasa tumepata ushindi wa mabao 7-1 ni faraja sana, hii imetokana na ushirikiano wa wachezaji na ninaamini wataweza kufanya hivyo katika mchezo ujao.
“Nimefurahishwa na uwezo wa Coutinho wa kufunga mabao matatu katika mchezo huo, ni sifa kwake kwa kuwa ameonesha ubora wake. Hata hivyo, ushindi huo unanikumbusha Kombe la Dunia mwaka 2014 katika hatua ya nusu fainali ambapo tulifungwa na Ujerumani,” alisema Dunga.
Mchezo unaofuata katika kundi B, Brazil watapambana na Peru ambao utakuwa wa mwisho kwa kundi hilo.