SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema wabunge wote wa upinzani wanaosusia vikao vya Bunge kwa kipindi chote
ambacho wamekuwa wakisaini na kuondoka bungeni bila kufanya kazi, hawatalipwa posho.
Alitangaza uamuzi huo bungeni jana baada ya Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango kuwasilisha Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Dk. Tulia alisema baada ya kutafakari kuhusu kinachoendelea kwa wabunge hao wa upinzani kususia vikao vya Bunge na kusaini bila kufanya kazi ni ukiukwaji wa kanuni.
“Kanuni ya 5 ya uendeshaji vikao vya Bunge, kifungu kidogo cha kwanza, inampa Spika mamlaka ya kuangalia uamuzi uliowahi kutolewa katika kipindi cha nyuma na kufanya uamuzi kwa suala lililopo,”alisema Dk.Tulia.
Alisema alipitia uamuzi mbalimbali ukiwamo wa mwaka 2008 uliotolewa na aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta kwa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), ambako wabunge hao walitoka bungeni na Spika aliamuru wasilipwe posho zao kwa muda wote ambao hawakufanya kazi bungeni.
“Kutokana uamuzi huo wabunge ambao wanaandika katika mahudhurio na kuondoka bila kufanya kazi yao hawatalipwa posho zao kuanzia siku walioanza kusaini na kuondoka pasipo kufanya kazi yenyewe,” alisema Dk.Tulia.
Uamuzi huo wa Naibu Spika unapingana na ule alioutoa wiki iliyopita, aliposema wabunge hao wana haki ya kuendelea kulipwa mshahara na posho zao, kwa vile malipo yao yapo kwa mujibu wa sheria.
Dk. Tulia alikua akizungumzia mwongozo ulioombwa Juni 2, mwaka huu na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe pamoja na Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy (CCM), ambaye alisema wabunge hao hawapaswi kulipwa Kwa sababu ni sawa na kuwalipa wabunge hewa.
Katika kuomba mwongozo wake, Dk. Mwakyembe alitaka kujua kama ni haki kwa wabunge hao kuendelea kulipwa, wakati Ibara ya 23 ya Katiba inasema mtu atalipwa ujira kulingana na kazi anayofanya.
Akitoa majibu wakati huo, Dk. Tulia alisema wabunge hao wataendelea kulipwa kwa kuwa malipo yao yapo kwa mujibu wa sheria.
Naibu Spika alirejea uamuzi wa kiti uliowahi kutolewa bungeni Aprili 27, 2016 katika mwongozo kama huo ulioombwa na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).
“Masharti hayo yamefafanua kuwa, mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge pamoja na kamati zake atalipwa posho kwa viwango vitakavyowekwa na Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Fedha na kanuni zake,” alisema.
Alisema, malipo ya mshahara kwa mbunge ni suala la katiba na sheria na kwamba malipo hayo hulipwa kwa kazi yake ya ubunge kama yalivyotajwa katika Ibara ya 73 ya Katiba.
“Malipo ya posho kwa mbunge yalianzishwa kwa mujibu wa Katiba na pia yamewekwa katika sheria ya uendeshaji wa Bunge sura ya 115, inayosema mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge pamoja na kamati zake atalipwa posho kwa kuzingatia kiwango kilichoweka.
“Pia si sahihi wala halali kwa mbunge kupokea posho na mshahara bila ya kufanya kazi, kama kiti kilivyoamua katikauamuzi nilioutaja vitendo vya kutoka ukumbini baada ya kusaini havikubaliki,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Tulia alisema iko haja kwa siku zijazo kufanya marekebisho sheria zilizopo kukabiliana na hali ya namna hiyo na kuweka utaratibu mahususi.
Dk. Tulia alisema, utaratibu huo utawezesha kila mbunge kulipwa posho baada ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa vile kusaini mahudhurio pekee haitoshi.