UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga, umesogeza mbele mpango wake wa kumpiga bei mshambuliaji wake mahiri Mzimbabwe, Donald Ngoma, kutokana na kukabiliwa na michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kutokana na uamuzi huo, Ngoma kwa sasa atasubiri hadi msimu ujao ili kutua klabu ya Al Ahly au Zamalek zote za Misri ambazo zinafukuzia saini ya mshambuliaji huyo.
Akizungumza na MTANZANIA, Mkurugenzi wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema uamuzi huo ulikuja baada ya kuona umuhimu wa mchezaji huyo kimataifa.
“Ni kweli tumeahirisha mpango huo kutokana na kukabiliwa na michezo ya kimataifa, hivyo kwa sasa Ngoma atasubiri hadi msimu ujao,” alisema Muro.
Hata hivyo, chanzo cha ndani ya klabu hiyo kilisema kuwa uongozi wa klabu hiyo unaweza kulazimika kumshawishi Ngoma aongeze mkataba wa mwaka mmoja kutokana na sababu za kibiashara.
“Unajua kama Ngoma asipoongeza mwaka mmoja anaweza kuondoka bure baada ya msimu ujao, hivyo ili biashara iende vizuri lazima ushawishi ufanyike.
“Uamuzi wowote unaweza kufanyika kwa sababu za kibiashara kama dau likiwa nono, lakini bado Yanga inamhitaji Ngoma kipindi hiki,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, chanzo hicho kilisema timu zinazomhitaji mchezaji huyo kwa sasa haziwezi kumtumia mchezaji huyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuwa mchezaji huyo tayari alicheza akiwa na Yanga.
“Sababu hii inaweza kuzifanya timu hizo kuwa tayari kusubiri hadi msimu ujao ndipo zimnunue mchezaji huyo ambapo Yanga haitakuwa tayari kumtoa bure hivyo italazimika kumpa mkataba,” kilisema chanzo hicho.