IMAM Ruhullah al-Musawy al-Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizaliwa mwaka 1900 katika ukoo wa wachamungu mjini Khomein, Kusini-Magharibi ya Tehran (Iran).
Babu yake na baba yake walikuwa wanazuoni. Baba yake, Ayatullah Mustafa, aliuawa na magaidi miezi mitano kabla ya kuzaliwa Ruhullah hivyo, akalelewa na mama na shangazi yake.
Alipokuwa na miaka 16, mama na shangazi yake walifariki dunia na kaka yake, Sayyid Murtaza (mashuhuri kwa jina la Ayatullah Pasandide) ndiye akawa na jukumu la kusimamia masomo yake. Ayatullah Pasandide alimfundisha Khomeini lugha ya Kiarabu na masomo mengine ya kimsingi.
Alipokuwa na miaka 18, Khomeini alipelekwa chuoni karibu na mji wa Arak. Mwalimu wake alikuwa Ayatullah Shaykh Abdul Karim Hairi.
Mwaka uliofuatia, Hairi alipokea mwaliko kutoka kwa wakazi na maulamaa (Wasomi)Â wa mji wa Qum kumtaka ahamie huko.
Mji wa Qum ulikuwa ni makao ya elimu na ziara. Shaykh Hairi alipofika mjini Qum akaanza kuratibu upya mpango wa hawza (chuo cha dini)Â ya Qum. Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza ya maendeleo kati ya hatua mbalimbali zilizouinua mji wa Qum kufikia kuwa ni mji mkuu wa maarifa ya Kiislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hatua ya mwisho na muhimu ya maendeleo ilikuwa ni mapambano ya taifa zima dhidi ya utawala wa kifalme wa Pahlavi ambayo yalianzishwa na Imam Khomeini (Khumayni) mwaka 1962 mjini Qum.
Tukiangalia umaarufu wa sasa uliompatia Imam Khomeini kama ni kiongozi mwanamapinduzi aliyepata mafanikio ya kipekee katika uwanja wa kisiasa, tusistaajabu kuona kwamba awali alikuwa maarufu kama mwandishi na mwalimu anayehusika na mambo ya kiibada.
Ayatullah Hairi aliaga dunia mwaka 1937 na chuo cha kidini kikawa kinasimamiwa kwa muda na jopo la wasaidizi wake watatu.
Imam Khomeini alikuwa akimfanyia kampeni Ayatullah Burujardi kupewa wadhifa wa uongozi akimtarajia kwamba atatumia fursa na wadhifa wake mkubwa wa kidini katika kupambana dhidi ya utawala wa Pahlavi.
Alishirikiana na Ayatullah Burujardi mpaka alipofariki mwaka 1962. Ingawa historia inamhesabu Ayatullah Burujardi kwamba alikuwa kiongozi mcha Mungu na mwendeshaji hodari lakini kutokana na sababu kadhaa hakuwa na harakati za kisiasa.
Baada ya kufariki Ayatullah Burujardi hakutokea hata mtu mmoja kushika cheo chake. Khomeini alisita kuruhusu jina lake lifanyiwe kampeni.
Lakini mwishowe akaitikia maombi ya masahibu zake, hii ikawa na maana kwamba alikuwa tayari kushika hatamu za uongozi na mamlaka ya kidini.
Ndipo hapo umashuhuri wa Imam Khomeini ukaenea mjini Qum na nchini kote Iran. Jambo lililokuwa muhimu zaidi ni kuwa tayari kuukabili utawala wa Shah katika wakati ambao watu wachache tu walithubutu kufanya hivyo.
Baadaye akawa anashughulikia mambo yaliyo muhimu zaidi. Hatua ya kwanza aliichukua Oktoba 1962 wakati Shah alipotangaza sheria ya kuondoa masharti ya kuwa Mwislamu na mwanamume katika kugombea uchaguzi wa mabaraza ya mikoa.
Imam Khomeini alijiunga pamoja na maulamaa wengine nchini kote kupinga vikali hatua hiyo; na hatimaye Shah akashindwa.
Hatua ya pili ilichukuliwa mwaka 1963 wakati Shah alipoanza kutangaza maazimio mapya kwa ajili ya kugeuza hali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya Iran. Maazimio hayo yalijulikana kama “Mapimduzi Meupe”.
Kura ya rai (referendum) ilifanywa kwa ulaghai mnamo Januari 26, 1963 ili kuunga mkono maazimio hayo.
Ili kuukomesha upinzani huo, utawala wa Shah ulipeleka askari wa miamvuli kushambulia Madrasa Fayziya Machi 22 1963 ambapo wanafunzi wengi waliuawa na madrasa yenyewe ikaharibiwa.
Imam Khomeini aliendelea kuushutumu utawala wa Shah kati ya miezi Machi na Mei mwaka 1963. Aliushambulia utawala wa Shah hasa kutokana na udhalimu wake, unyenyekevu wake mbele ya Marekani na ushirikiano wake na Israel. Mkabala huo ulifikia kilele kipya kabisa mwezi wa Juni ulioandamana na mwezi wa Muharram.
Mwezi wa Kiislamu wa Muharram huadhimishwa kila mwaka kukumbuka ushahidi wa Imam Husayn AS, mjukuu wake Mtume Muhammad SAW, ambaye alipambana dhidi ya udhalimu na upotevu wa Yazid.
Mwezi huu huadhimishwa ili kuhuisha mfano huo kwa kupambana dhidi ya madhalimu wa kila zama. Siku ya Ashura (tarehe 10 Muharram), Imam Khomeini alitoa hotuba ya historia mjini Qum na akazidi kuushutumu utawala wa Shah na akamwonya Shah asitende jambo ambalo litawafanya watu wamlazimishe ahame nchini na wafurahiye kuondoka kwake.
Siku mbili baadaye alikamatwa na kupelekwa Tehran.
Kukamatwa kwa Imam Khomeini kulizidisha upinzani wa umma na mapambano yao makubwa yakautingisha utawala wa Shah. Katika miji ya Qum, Tehran, Shiraz. Mash’had, Kashan na miji mingineyo, waandamanaji wasiokuwa na silaha walikabiliana na askari wa Shah.
Askari hao walipewa amri ya kufyatua risasi na kuua papo hapo na matokeo yake watu wasiopungua 15,000 waliuawa katika muda wa siku chache. Tukio hilo ambalo lilitokea tarehe 15 Khordad 1342 (kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawasawa na Juni 5 1963), likafungua ukurasa mpya wa historia ya Iran. Tukio hilo lilimwaminisha Imam Khomeini kama ni kiongozi wa taifa na mwenye kuwakilisha matakwa ya umma.
Imam Khomeini alianzisha mapambano dhidi ya Shah na vibaraka wake kufuatana na msingi wa itikadi ya Kiislamu na akawaelekeza watu kuendeleza harakati zao chini ya uongozi wa maulamaa na mashekhe badala ya kusimamiwa na vyama visivyokuwa vya kidini ambavyo vilipoteza imani ya watu baada ya kupinduliwa Musaddiq. Kwa hivyo, mzinduko wa Khordad 15 ukawa ni msingi ulioleta Mapinduzi ya Kiislamu.
Ingawa upinzani ulikandamizwa lakini wananchi na maulamaa walikataa kuvumilia kufungwa kwa Imam Khomeini.
Machafuko yalienea nchini kote na maulamaa wengi wakakusanyika mjini Tehran kusisitiza kuachwa huru kwa Imam Khomeini. Hatimaye, Imam Khomeini aliachiwa huru Aprili 6 1964.
Imam Khomeini pamoja na harakati aliyoipa sura havikusahauliwa katika Iran. Mfano wake uliwavutia maulamaa wengi na vikundi vingi, mfano ambao uliendelea kuimarisha misingi aliyoiweka katika miaka ya 1963 na 1964 na ukasababisha harakati za Kiislamu zisizo kuwa na mfano zipanuke na zikue.
Kwa hivyo, ikawa ni jambo la kawaida kwa Imam Khomeini kujitokeza haraka kuwa kama kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Tangu kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini ameendelea kushika wadhifa wake kwa busara na hekima na kuliongoza taifa kufikia shabaha yake.