Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajiwa kukutana wakato wowote kuanzia sasa kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho.
Hata hivyo, taarifa za ndani ziliiambia MTANZANIA kuwa katika hatua za awali tayari chama hicho kimepanga mkutano huo kufanyika Julai 20 au 21 mwaka huu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema kikao hicho ndicho kitaamua lini mkutano huo utafanyika.
Sendeka alisema ajenda kuu itakuwa ni kukabidhiwa chama kwa Rais Dk. John Magufuli kama ilivyo utamaduni wa chama hicho.
“Kikao cha CC ndicho chenye maamlaka ya juu na kitakutana wakati wowote na kupanga tarehe ya mkutano mkuu wa chama chetu,” alisema Sendeka.
Kikao cha mwisho cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kilikuwa Februari 3, mwaka huu Ikulu ya Chamwino, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Katika kikao cha Dodoma wajumbe walishindwa kuafikiana tareehe ya mkutano mkuu jambo ambalo liliibua mjadala mzito hasa baada ya kuelezwa kuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete hakuwa tayari kukabidhi chama kwa kile alichodai hakuna fedha kwa sasa.