Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chadema kwa mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema anasononeshwa na hali ya maisha ya Watanzania inavyozidi kuwa ngumu hivi sasa huku bei za bidhaa zikizidi kupanda na hata kuadimika.
Alitoa mfano wa kuadimika sukari ambayo ni bidhaa muhimu katika kipindi hiki kuelekekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Taarifa ya Lowassa Dar es Salaam jana iliyosainiwa na msemaji wake, Abubakar Liongo, ilikuwa maalum kwa ajili ya kuwatakia mfungo mwema waumini Waislamu wanaotarajia kuanza mfungo kesho.
“Kwa niaba ya mke wangu Regina na mimi binafsi, nachukua nafasi hii kuwatakia waislam wote nchini kila la kheri na baraka tele kwenye mwezi huu mtukufu. Nafahamu Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni kipindi muhimu kwa waislam kuwa karibu na mola wao.
Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwaomba waislam kutumia mwezi huo mtukufu kuliombea taifa amani, upendo na mshikamano.
“Lakini zaidi tusisahau kuomba haki na hamu ya Watanzania kuona mabadiliko ya siasa yanafanyika kwa amani na wale wenye ulevi wa kuminya haki hiyo, hawapati tena nafasi kutekeleza uovu wao, tusiache kuwaombea viongozi wetu wawe na hofu ya Mungu.
“Ninawaomba wafanyabiashara kupunguza bei ya bidhaa hususan zile muhimu katika mwezi huu, ili ndugu zetu waislam watimize Ibada yao vizuri.
Waislamu wa Tanzania wanaungana na wenzao kote duniani katika kutimiza moja ya nguzo tano za kiislam kwa kufunga Ramadhan.