MSHAMBULIAJI wa FC Platinum ya Zimbabwe, Walter Musona anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya mazungumzo ya mwisho na kabu ya Yanga.
Ujio wa Musona katika kikosi hicho ni baada ya Wazimbabwe Donald Ngoma na Thabani Kamusoko kumpendekeza mshabuliaji huyo na kuwaambia viongozi kama watafanikiwa kunasa saini yake watakuwa wameimarisha safu ya ushambuliaji.
Taarifa za uhakika kutokana ndani ya klabu hiyo, zinasema kwamba mchezaji huyo anatarajia kutua nchini leo kwa ajili ya kukamilisha taratibu za usajili.
Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa ripoti ya kocha mkuu Hans Van De Pluijm, ilitaka kuongezwa mshambuliaji mmoja mwenye uwezo mkubwa atakayesaidiana na akina Amis Tambwe na Ngoma, hivyo ujio wa Musona ni maagizo ya kocha huyo.
“Musona anatua nchini kesho (leo) kwa ajili ya makubaliano ya suala zima la mkataba na baada ya kuafikiana huenda akasaini mkataba wa miaka miwili kukitumikia kikosi cha Yanga,” alisema kigogo huyo.
Alisema pia ujio wa mshabuliaji huyo utawasaidia kutokana na klabu ya Zamaleck na Al Ahly za nchini Misri kuwa kwenye mipango ya kumsajili Ngoma.