KILA taifa lina vitu katika jamii ya vyakula ambavyo vikiguswa basi nchi nzima hutikisika na kwa kawaida Serikali haifanyi mchezo katika vitu hivyo maana inajua kuwa itasakamwa na wakati mwIngine hata kuangushwa kwa ghadhabu ya wananchi.
Sudan aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jaffar Numeir alifanyiwa maandamano makubwa na wananchi wa nchi hiyo kwa kupandisha bei ya mkate, wakati nchi nyIngine sukari ni jambo kubwa ambalo huwaunganisha wananchi dhidi ya Serikali.
Kwa kwetu Zanzibar ni mchele. Lakini kulikuwa na wakati Serikali ilibana kwenye mchele, unga wa ngano na sukari na ikawa mgao ni wa kila wiki kwa kile kilichoitwa “Ukoo” na kila ukoo yaani familia ilikuwa na kadi yake maalumu ya kununulia bidhaa hiyo. Wananchi walichoka sana na ndio maana lilipokuja wazo la kuunganisha vyama vya ASP na TANU hilo likakubalika haraka.
Haikuwa kwamba ni mapenzi ya udugu wala nini. Ni dhiki ya chakula pamoja na maonevu ya Serikali kwa raia kwa kukamatwa kamatwa ovyo ndipo Chama cha Mapinduzi kikazaliwa, maana ilikuwa ndio njia ya kuonesha hasira kwa Serikali.
Hata Tanzania Bara kulikuwa na hasira kubwa ya umma kutokana na sera za Ujamaa na Kujitegemea za Mwalimu Nyerere na chakula kwa ujumla na bidhaa nyingine nyingi zikawa ni shida na ndio moja ya sababu kuu wananchi kushinikiza kwanza kufutwa kwa Sera ya Ujamaa kupitia Azimio la Zanzibar mwaka 1992 na mwaka huo huo nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi.
Huko nyuma, chumvi ilikuwa ni bidhaa muhimu sana, lakini kutokana na kukua na kuenea tamaduni na kuchanganyika, sukari imekuwa ni bidhaa inayotumiwa na kila jamii ya Kitanzania na hapana shaka kukosekana au kupungua kwake kunahisiwa kote nchini, pwani na ziwani.
Serikali inasema inajua mahitaji ya nchi ya sukari. Lakini sijui kama inajua kuwa au inatia hesabu kuwa pia mahitaji hayo ni pamoja na kwamba sukari inayoingizwa na kuzalishwa nchini pia husafirishwa katika miji ya nchi jirani zetu tunazopakana nazo.
Akijibu swali la papo kwa papo bungeni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema upungufu uliopo unaweza kudhibitiwa kwa kuagiza sukari ya zaida na kuwa Serikali imekwisha chukua hatua kuziba pengo hilo. Naona sasa sijui kama alikuwa akijua hali halisi ilivyo au alinyimwa taarifa na wasaidizi wake.
Na pia inanishangaza na naanza kujiuliza iwapo Serikali inajua kwa hakika hata kiwango kinachozalishwa na viwanda vya ndani, maana Serikali hiyo hiyo ilipotoa amri ya kupiga marufuku sukari ya nje, wengine tuliamini makeke yale yana mashiko na Serikali inakijua inachokifanya.
Dhana ya kuzuia kitu kutoka nje ili kitu cha ndani kiuzwe au kizalishwe huitwa “protectionism” yaani “ulindaji”. Kwa kawaida katika uchumi wa soko dhana hii ni mbaya na huwa haikubaliki, lakini hufanywa na nchi kiubishi kulinda bidhaa zake au kuvipa nguvu viwanda vyake.
Hapana shaka ulindaji huu uambatane na hali halisi ya kupatikana kwa bidhaa yenyewe lakini pia na ushindani kwa ubora wa bidhaa hiyo. Isiwe tu kulinda bidhaa za nje lakini viwanda vya ndani havina uwezo wa kuziba pengo na bidhaa zake ni za kiwango cha chini.
Kwa umuhimu na ulazima wa soko hili la sukari hapa Tanzania, huwa linadhibitiwa na wafanyabiashara wakubwa na matajiri sana. Hawa hupata vibali vya kuagiza na wakati mwingine kwa mgao yaani “quota” na hawa wafanyabishara hupigana vikumbo na kufanyiana matendo hata ya kiharamia baina yao katika kuwania soko.
Hili Serikali naamini ingepasa ilijue. Ijue kama ilivyojua mambo yalivyokuwa yakienda katika biashara ya petroli na mwisho kufanywa uamuzi wa uagiziaji wa pamoja (bulk importation). Nashangaa mno sasa hivi nikiona Serikali inahamanika katika suala hili.
Sikutaraji kuwa suala hili lingesababisha hata kuingiliwa na Rais Magufuli kwa kutoa hata hotuba kali ya kutaka walioficha bidhaa hiyo waitoe na hata kuamuru kuwa wakamatwe kwa kuficha na washitakiwe kwa kuhujumu uchumi. Ilikuwa haina haja ya kufika kote huko.
Rais Magufuli akachagua kuizungumza habari hiyo mbele ya umma baada ya kile kilichosemwa kuwa alisimamishwa njiani na wananchi wa Manyara akiwa njiani kwenda Arusha, jambo ambalo mimi naona lilipangwa kutokea. Kwa hivyo hii ni “sukari ndani ya siasa”
Inakuwaje kuwa Rais wetu ahusike katika kila kitu hata kukemea ufichwaji wa sukari? Kwani hivi wachumi wake hawakumwambia kuwa hilo lingetarajika kwamba popote pale Serikali inapolazimisha kitu basi thamani ya kitu hicho hupanda na mara inakuwa adimu ili wenye nacho wafaidike?
Maana ingekuwa ni “siasa katika sukari” basi ningeelewa na hii ingekuwa kwamba sukari imeadimika tu wenyewe kwa misingi ya uhaba na upatikanaji na hapa wanasiasa kujitokeza na kudai ipatikane. Lakini sivyo, ni wanasiasa na hususani Serikali imefanya sukari iadimike.
Ukweli ni kuwa jambo hili limesemewa sana na wataalamu wengi na hata Bunge kulitolea kauli lakini Serikali wakati wa Rais Kikwete lakini Dk. Magufuli akiwa ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri walilikalia na halikufanyiwa uamuzi wa maslahi ya muda mrefu.
Mimi naona hili ni kucheza na akili za Watanzania kwa watu kutaka kutia sukari katika siasa. Watanzania wanajua kabisa kuwa kama hili linasimamiwa vyema halingepaswa kabisa kufika hapa tulipofika, isipokuwa ni kukosa usimamizi imara.
Sukari inapokuwa nyingi katika chakula au kinywaji chochote hakiliki wala hakinyweki na hii kwenye siasa hivi sasa imekuwa ni mno. Pia wapo ambao pia wanataka kufanya siasa katika sukari, ili wafaidike na kupanda chati, lakini letu sisi jicho tu. Kila taifa lina vitu katika jamii ya vyakula ambavyo vikiguswa basi nchi nzima hutikisika na kwa kawaida Serikali haifanyi mchezo katika vitu hivyo maana inajua kuwa itasakamwa na wakati mwingine hata kuangushwa kwa ghadhabu ya wananchi.