MAULI MUYENJWA NA FLORIAN MASINDE, DAR ES SALAAM
WAKAZI wa eneo la Mloganzila, Kibamba katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam wameanza kulala nje kutokana na ubomoaji wa nyumba zao unaoendelea.
MTANZANIA jana ilishuhudia wananchi hao wakiwa maeneo hayo wengi wakiwa wameanza kulala nje kwa siku ya pili.
Wananchi hao wanawalalamikia viongozi wa serikali za mitaa kwa kushirikiana na matapeli na kuwadhulumu fedha zao kwa kuwauzia viwanja vyenye migogoro.
Mmoja wa waathirika wa ubomoaji huo, Elisha Isha alisema wanaiomba serikali iwapatie msaada wa kibinadamu kikiwamo chakula na mahema kwa kuwa hawana mahali popote pa kwenda wakati huu.
“Vyakula vyote vimeharibika hatuendi kazini, watoto shuleni hawaendi na mpaka sasa hakuna msaada wowote tulionao na hatujui mahali pa kwenda.
“Viongozi waliokuwapo awali walijua matatizo haya lakini hawakutwambia na sasa hawaonekani wameingia mitini,” alisema Isha.
Naye Diwani wa Kata ya Kwembe, Dweza Kolimba (Chadema) alisema amesikitishwa na hali hiyo ya wananchi hao kudhalilika kiasi hicho wakati tayari walikwisha kujipatia makazi.
Alisema mpaka sasa hakuna msaada wowote walioupata na kitengo cha maafa hakijafanya lolote hata kufika maeneo hayo.
“Tulichofanya ni kuwagundua wakazi walioathirika lakini makosa yalifanywa na viongozi wa kwanza ambao walijua matatizo ya maeneo haya lakini kwa kuwa walikuwa wanapata asilimia 10 walitamani fedha na kuacha utu wa mtu na mwenye eneo anataka eneo lake na watu wanavunjiwa,” alisema Kolimba.
Mmiliki wa eneo hilo, Henry Kashangaki alisema serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa vile ilikuwa inajua eneo hilo ni lake lakini ilitoa vibali kupitia serikali za mitaa na watu wakaanza kuuziana na kutapeli wananchi wasiokuwa na hatia.
Nyumba zaidi ya 400 zinatakiwa kuvunjwa katika eneo la ekari 33 mali ya Kashangaki. Eneo hilo lilivamiwa na watu 10 ambao baadaye waliwauzia wengine zaidi ya 600 ambao ndiyo wameathiriwa na ubomoaji huo.