MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) amesema aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikuwa ni jipu lililojificha Ikulu.
Alisema hatua ya kutumbuliwa na Rais Dk. John Magufuli ni sahihi kwa vile imeenzi kwa vitendo kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa Ikulu ni mahali patakatifu.
Kauli hiyo aliitoa bungeni jana, alipokuwa akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Migugo na Uvuvi ya mwaka 2016/17 ya Sh bilioni 275.06.
Alisema pia kuwa hatua ya kuimarisha sekta ya kilimo huenda sambamba na uimarishaji wa maisha ya wakulima.
“Mheshimiwa Mwenyekiti hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti tangu ilipoundwa Serikali ya Awamu ya Tano, kwa hali hiyo ninapenda kumpongeza Rais Magufuli kwa kumtumbua jipu aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi Sefue).
Alimtaka Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba kuhakikisha anatumbua majipu yaliyopo katika wizara yake likiwamo la wakulima hewa kilimo kiweze kukua.
Lugola alisema Wizara ya Kilimo ni wizara nyeti ambayo inatakiwa kuangaliwa kwa umakini, lakini ina wakulima hewa, hivyo waziri anatakiwa kuwatumbua.
“Jimboni kwangu vocha za pembejeo zenye thamani ya Sh milioni 46.3 zimetolewa kwa wakulima ambao hawapo.
“Kuna mmoja yupo Mwanza wamemuandika yupo kwenye jimbo langu kuwa ni mkulima wakati siyo kweli.
“Kna mwingine na mdogo wake wapo kata nyingine wamewaandikwa kwenye vocha za pembejeo, Nchemba tumbua jipu la wakulima hewa vinginevyo hatutapata mali shambani,” alisema
Akizungumzia kilimo cha pamba, alisema kuna kila sababu ya waziri huyo wa kilimo kwenda kutumbua majipu hasa katika mbegu feki za pamba zisizoota za Quton na ambazo zimekuwa zikisababisha kushuka kwa zao hilo mwaka hadi mwaka.
“Hii kampuni ya mwekezaji ni feki na wabunge wamepiga kelele kwenye bodi ya pamba wanamkumbatia… huyo ni jipu ikiwezekana waziri ukitoka hapa nenda ukatumbue jipu la kampuni ya Quton,” alisema Lugola
Mwigulu na bajeti bil 275.06/-
Awali akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchema, aliomba Sh bilioni 275.06 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Upinzani
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Magdalena Sakaya, alisema kwa kipindi cha mwaka wa fedha unaomalizika Bunge liliidhinisha Sh bilioni 60.373 kwa wizara ya mifugo na uvuvi (sasa ni idara) zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo, kati ya hizo Sh bilioni 19. 398 zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Alisema taarifa ya Wizara inaonyesha hadi kufikia Machi 31, mwaka huu, wizara ilikuwa haijapokea hata Sh moja kati ya Sh bilioni 19.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.