KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajiwa kukutana kesho mjini hapa, MTANZANIA limeelezwa.
Chanzo cha kuaminika kimelidokeza gazeti hili kuwa pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitajadili maandalizi ya mkutano mkuu maalumu, ambao unatarajiwa kufanyika Juni mjini hapa.
Kwamba katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ataachia ngazi na kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli kama utamaduni wa chama hicho ulivyo katika kukabidhiana kijiti cha uongozi.
Tangu wiki iliyopita vikao kadhaa vya Sekretarieti vimekuwa vikiendelea mjini hapa, vikiwahusisha watendaji wa juu wa CCM pamoja na makatibu wa idara husika ambao huteuliwa na mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Kikao hicho cha kesho pia kinatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Magufuli, ambaye tayari yupo mjini hapa alipokuja kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi – Mei Mosi.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nao wataungana na viongozi wa ngazi za juu wa CCM katika kikao hicho.
Katika kikao cha kesho, Kamati Kuu pia itajadili na kupitisha majina ya wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka miongoni mwa wabunge wa CCM.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zilieleza kuwa kikao hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake Kikwete, ambapo wabunge walioomba nafasi hizo, majina yao yatapelekwa kwa wabunge wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.
“Wabunge wana nafasi 10 za NEC na unajua waliokuwa wajumbe walishapoteza sifa za kuwa wajumbe, hivyo kwa kawaida kila Bunge jipya linapochaguliwa ni lazima uchaguzi ufanyike.
“Pamoja na kupitia majina ya wabunge waliojaza fomu, pia CC itajadili majina ya wabunge walioomba nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM ambapo kuna wajumbe zaidi ya watatu wamejaza fomu,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa wabunge wanaotajwa kuwania nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM yumo Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, ingawa wapo wabunge wengine ambao kwa pamoja watachujwa na kikao cha kesho.
Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM anayemaliza muda wake ni Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama.
Waliochaguliwa Bunge la 10
Aprili 15, mwaka 2011, wabunge wa CCM walichagua wajumbe 10 wa NEC akiwamo aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, ambaye alichaguliwa kwa kupata kura 104.
Katika uchaguzi huo, baadhi ya wagombea walikuwa wanawatumia wabunge wenzao kuwafanyia kampeni, huku wengine wakikodi wapigadebe kutoka Dar es Salaam.
Katiba ya CCM inaruhusu wabunge wa chama hicho kuwachagua wajumbe 10 kuingia NEC kutoka miongoni mwao.
Mbali na Sitta, wabunge wangine walioshinda ni Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, Nimrod Mkono (Butiama), aliyekuwa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Wengine waliochaguliwa ni wabunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki, Munde Tambwe, Faida Mohamed Bakari, na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim.
Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye kwa sasa anawakisha Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.
Wabunge walioanguka katika uchaguzi huo ni waliokuwa wabunge katika Bunge la 10, Brigedia Jenerali Mstaafu, Hassan Ngwilizi (Mlalo), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini), aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Athman Mfutakamba, Dk. Charles Tizeba (Buchosa) na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro).
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile, Ahmed Salum Ali (Solwa), Yahya Kassim Issa (Chwaka), Mwanahamisi Kassim Saidi (Viti Maalumu), Martha Mlata (Viti Maalumu) na Saidi Mussa Zubeir (Fuoni).