KOCHA wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amesema kikosi chake hakitoathirika kutokana na kukosekana kwa beki mahiri wa timu hiyo, Hassan Kessy, wakati kitakapocheza dhidi ya Azam kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Mei Mosi, Dar es Salaam.
Simba ambayo ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza michezo 25, inatarajia kucheza mchezo huo bila ya beki huyo ambaye alipewa adhabu ya kukosa michezo mitano baada ya kufanya rafu mbaya dhidi ya mchezaji wa Toto Africa, Edward Christopher.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mayanja alisema kuwa mfumo wake uwanjani ungetetereka endapo ingewakosa wachezaji watatu muhimu lakini si mchezaji mmoja.
“Hivi karibuni tunatarajia kuweka kambi visiwani Zanzibar sababu kubwa ni kupata muda mwingi wa kufanya maandalizi, hata hivyo kikosi changu kipo tayari kwa mapambano licha ya kumkosa beki huyo.
“Ni mchezo wa ligi ambao ni muhimu kwetu ili kupata ushindi na kujihakikishia kuwemo katika mbio za ubingwa msimu huu, licha ya kupoteza dhidi ya Toto,” alisema Mayanja.
Mayanja alisema kuwa bado kikosi chake kina hamasa, hakijakata tamaa na kuahidi kuwa kitapambana hadi dakika ya mwisho.