HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, imesaini mkataba na Kampuni ya MS/H Gauff Ingenieure GMBH & Co, KG – JBB ya Ujerumani kwa ajili ya kutoa huduma za ushauri elekezi katika usimamizi wa ujenzi wa miradi ya Mpango wa Maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam (DMDP).
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jacob Boniface alisema mkataba huo utadumu hadi mwisho wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Alisema mradi huo, unatarajia kugharimu Sh bilioni 11.6.
Alisema kampuni hiyo, itakuwa na jukumu la kuhakikisha kazi zitakazofanyika zinakuwa kwenye mpangilio uliokubalika kwa kuzingatia ubora na thamani ya mradi ili wananchi wa manispaa hiyo na jiji la Dar es Salaam wanufaike.
Alisema Halmashauri ya Kinondoni ina miradi 11 inayogusa maeneo ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, zinazolenga kupunguza msongamano, uboreshaji wa miundombinu maeneo yasiyopangwa, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, uimarishaji wa mifumo ya mapato ya utawala bora ya taasisi na usimamizi wa taka ngumu.
“Upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu waelekezi, kati ya miradi yote ya awamu ya kwanza na ya pili, miradi mitano ya barabara itakayotekelezwa kuanzia sasa haihitaji ulipaji wa fidia na barabara sita zitajengwa baada ya manispaa kulipa fidia,” alisema Jacob.
Alisema kwa kushirikiana na baraza lake la madiwani na Serikali kuu, wadau wengine na wabunge watafanya jitihada za kutafuta fedha za kulipa fidia ili miradi ianze kutekelezwa na kukamilika.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Thorsten Seiz alisema watahakikisha wanafanya kazi hiyo kwa umakini na uadilifu ili wananchi wa Dar es Salaam wanufaike na miradi hiyo.