Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Shirika la CAMFED Tanzania limesema limefanikiwa kuwasaidia wasichana 509,033 kupata elimu ya msingi na sekondari nchini, wakilenga kusaidia watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu.
Hayo yamebainishwa na Novemba 12, 2024, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa CAMFED Tanzania, Anna Sawaki, katika mkutano wa kimataifa wa ubora wa elimu.
Kwa zaidi ya miaka 15, CAMFED imekuwa ikishirikiana na serikali ili kuhakikisha kila mtoto wa kike anayekabiliwa na changamoto za kifedha na kijamii anapata elimu bora. Sawaki alieleza kuwa shirika lina miradi maalum ya stadi za maisha, inayolenga kuwasaidia wasichana hawa kudumu na kufanikiwa katika masomo yao.
“Mbali na elimu ya msingi na sekondari, tumesaidia wasichana 5,632 kufikia elimu ya juu kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo Tanzania (HELSB),” alisema Sawaki.
Pia alibainisha kuwa CAMFED inaendesha miradi katika mikoa 10 na halmashauri 35, huku wakitarajia kufika halmashauri 41 ifikapo mwaka ujao.
Sawaki aliongeza kuwa shirika linatekeleza programu za ushauri na stadi za maisha, ambazo zinahusisha wasichana walionufaika na CAMFED kurudi mashuleni kusaidia wanafunzi wengine ili kuwapa motisha ya kuendelea na masomo yao.