32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watahiniwa 557,731 kufanya Mtihani wa kidato cha Nne mwaka 2024

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Dar es Salaam – Jumla ya watahiniwa 557,731 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, ambapo kati yao watahiniwa wa shule ni 529,321 na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,410.

Akizungumza leo Novemba 10, 2024, jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed, alifafanua kuwa mtihani huo utaanza kesho, Novemba 11, na kumalizika Novemba 29, 2024, ukifanyika katika shule 5,585 za sekondari na vituo 961 vya watahiniwa wa kujitegemea.

“Kati ya watahiniwa wa shule 529,321 waliosajiliwa mwaka huu, wavulana ni 250,562 ambao ni sawa na asilimia 47.34, na wasichana ni 278,759, sawa na asilimia 52.66,” alisema Dk. Mohamed.

Aliongeza kuwa watahiniwa wa shule wenye mahitaji maalum ni 1,088, wakiwemo wenye uoni hafifu, wasioona, wenye ulemavu wa kusikia, akili, na viungo vya mwili. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, walio na mahitaji maalumu ni 18, wakiwemo wenye uoni hafifu na wasioona.

Dk. Mohamed alisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti na usalama wa vituo vya mtihani, akiwataka wasimamizi wa mitihani kufanya kazi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Wasimamizi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni na miongozo waliyopewa ili kila mwanafunzi apate haki yake,” alisema. Pia alisisitiza kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum wanastahili huduma maalum kama mitihani ya maandishi ya nukta nundu kwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu.

Aidha, Dk. Mohamed aliwaonya wanafunzi dhidi ya vitendo vya udanganyifu, akisema, “Mwanafunzi yeyote atakayebainika kufanya udanganyifu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.”

Pia, aliwakumbusha wamiliki wa shule kuwa wanapaswa kuacha wasimamizi wa mitihani wafanye kazi yao kwa uhuru, huku akisisitiza kuwa baraza halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya vituo vya mitihani vitakavyokiuka mwongozo wa usimamizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles