26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

ACT-Wazalendo yapendekeza Kiswahili kutumika kama Lugha ya kufundishia

Na Elizabeth Zaya, Dar es Salaam

Chama cha ACT-Wazalendo kimeiomba serikali kubadili sera ya elimu ili lugha ya Kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu, huku Kiingereza na lugha nyingine zifundishwe kama masomo.

Waziri Kivuli wa Elimu wa chama hicho, Hamidu Bibali, alisema kutumia Kiswahili katika mfumo wa elimu kutarahisisha usambazaji wa taarifa, maarifa, na ujuzi kwa urahisi zaidi. Pia, alipendekeza kuanzishwa kwa mchakato wa kutafsiri na kutunga vitabu kwa Kiswahili ili kuwezesha upatikanaji wa rejea za kutosha.

“Lugha ya Kiswahili imekuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na kuwa na siku maalum,” alisema Bibali. “Kiswahili sasa kinakadiriwa kuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 500 duniani, na ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.”

Bibali alieleza kuwa Sera na Mtaala wa Elimu ya mwaka 2023 hauelezi wazi lugha ya kufundishia na kujifunzia, na kwamba kuna mkanganyiko mkubwa ambapo baadhi ya shule za umma na za binafsi zinatumia Kiingereza au Kiswahili kufundishia, huku sekondari zikitegemea zaidi Kiingereza.

“Lugha ni nyenzo muhimu katika mchakato wa kujifunza,” alisema Bibali. “Tafiti zinaonesha kuwa mtoto anaelewa zaidi akifundishwa kwa lugha yake kuliko lugha ya kigeni.”

Bibali alibainisha kuwa watoto wanashindwa kujibu maswali na kufeli mitihani kwa sababu ya kushindwa lugha. “Mtoto anapitia mchakato mrefu, asome kwa Kiingereza, atafsiri kwa Kiswahili, afikiri kwa Kiswahili, kisha abadili fikra hiyo kwenda Kiingereza,” alieleza.

Alisema kuwa mataifa yaliyoendelea kama Japan, China, India, Uingereza, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani, Ufaransa, na Korea Kusini yametumia lugha zao katika mifumo ya elimu. “Kumekuwa na hoja za muda mrefu kuwa Kiingereza ni lugha ya biashara, teknolojia, na ya kimataifa, lakini hakuna sababu ya kuendelea kutumia Kiingereza au lugha nyingine katika kutoa elimu nchini.”

“Kiswahili kina ukwasi wa maneno na kinajitosheleza. Maendeleo ya teknolojia yameondoa kabisa vikwazo vya mawasiliano, na sasa biashara yoyote inaweza kufanyika bila utegemezi wa lugha fulani,” alisema Bibali.

Bibali alihitimisha kwa kusema kuwa hakuna sababu yoyote ya Tanzania kutotumia Kiswahili kama lugha rasmi ya kujifunzia na kufundishia mpaka chuo kikuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles