Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema itahakikisha inaongeza wawekezaji kwenye maeneo ambayo yako wazi ili kuongeza matumizi ya gesi asilia viwandani na majumbani.
Akizungumza Julai 11, 2024, na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PURA, Halfani Halfani, alisema kuwa PURA ina majukumu ya kusimamia na kudhibiti shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli.
Amesema kuwa jukumu la PURA, chini ya kifungu Na. 12 cha Sheria ya Petroli ya 2015, ni kumshauri Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Petroli juu ya mambo yanayohusu mkondo wa juu wa Petroli nchini.
“PURA tunajukumu la kusimamia shughuli zote za mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika kwa ajili ya soko la nje ya nchi,” alisema Halfani.
Amesema kwa muda mrefu wamekuwa hawana wawekezaji wa kutosha hivyo watahakikisha wanaongeza wawekezaji hao katika maeneo ambayo yapo wazi.
Halfani alitaja mafanikio yaliyopatikana kwenye gesi asilia kuwa ni pamoja na kuchangia kwa wastani wa asilimia 50 ya umeme unaozalishwa nchini, kuongeza matumizi ya gesi asilia viwandani, majumbani, na kwenye magari.
Amesema Watanzania zaidi ya 1,428 wamepata ajira za kudumu na za muda katika miradi ya ufuatiliaji wa uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
“Kuanzishwa kwa kanzidata ya watoa huduma wa Kitanzania ambapo kampuni za watu zaidi ya 2,000 wamesajiliwa,” alisema.
Akizungumzia maonesho hayo, Halfani alisema kuwa awali yalikuwa kama gulio lakini kwa sasa yameboreshwa na kuwa na hadhi ya kimataifa. Ameipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kusimamia na kuyawezesha maonesho hayo.
Amewataka wawekezaji wenye uwezo kuwekeza nchini wafike kwa sababu Tanzania ni sehemu salama kwa biashara na uwekezaji.