25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Maandalizi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Iramba yakamilika

Seif Takaza na Hemed Munga, Iramba

Maandalizi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Iramba, mkoani Singida, yamekamilika kwa asilimia 100.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Suleiman Mwenda, mwenge huo utakimbizwa kilometa 68.1, ambapo utatembelea, kuona, kuweka mawe ya msingi ikiwemo kuzindua miradi iliyogharimu bilioni 5.084.”

Ametaja miradi itakayopitiwa na kutembelewa ni pamoja na mradi endelevu wa maji katika kijiji cha Makunda Uliyang’ombe uliozinduliwa mwaka jana, uwekaji wa jiwe la msingi katika kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti kijiji cha Kyengege, na ujenzi wa chuo cha ufundi stadi (VETA) eneo la Salala, kata ya Old Kiomboi.

Miradi mingine ni ujenzi wa shule mpya iitwayo Iramba Sekondari iliyopo kata ya Old Kiomboi, ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 1.5, na ujenzi wa majengo ya huduma ya afya ikiwemo mitambo ya kuzalisha hewa ya oksijeni, jengo la mama na mtoto, na jengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya Kiomboi.

“Natoa wito kwa wananchi wote, watumishi wa umma, taasisi mbalimbali na viongozi wa dini kujitokeza kwa wingi kuushangilia Mwenge wa Uhuru popote utakapo pita wilayani kwetu,” amesema Mwenda.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali wilaya yetu kwa kuipatia fedha nyingi ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Mwenge wa Uhuru utapokelewa wilayani Iramba katika kijiji cha Maluga mwezi Julai 9, mwaka huu ukitokea wilaya ya Singida. Hata hivyo, Mwenge huo ulipokelewa Julai 5 na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles