Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Dk. Jim Yonazi amesema wamejipanga kuwafikia wananchi wanaopata huduma katika banda jumuishi la ofisi hiyo lililopo kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba.
Akizungumza leo Julai 4,2024 na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali amesema watahakikisha wananchi wanapewa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu ofisi hiyo pamoja na taasisi zilizo chini yake.
Dk. Yonazi ametembelea banda la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Fedha na taasisi zake, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Kampuni ya simu ya Halotel pamoja na Shirika la Posta.
Ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kutembelea banda hilo na kupongeza namna watumishi wa ofisi hiyo wanavyoendelea huwahudumia wananchi na wadau wanaofika huku akiwasihi watumishi kuendelea kuzingatia weledi katika utoaji huduma na elimu kwa umma.
“Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya uratibu pamoja na huduma zinazotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu hivyo, wananchi na wadau mbalimbali wayatumie maonesho kama fursa ya kujifunza kuongeza uelewa,” amesema Dk. Yonazi
Maonesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanaongozwa na kaulimbiu isemayo; ‘Tanzania mahali sahihi pa biashara na uwekezaji.