Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Jumla ya watahiniwa 113,504 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, kati yao watahiniwa wa shule ni 104,449 na wakujitegemea ni 9,056.
Pia, jumla ya watahiniwa 11,552 wamesajiliwa kufanya mtihani wa ualimu kuanzia utakapoanza Mei 6, hadi Mei 20, mwaka huu.
Akizungumza leo Mei 5 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania(NECTA), Dk. Said Mohamed, amesema kati ya watahiniwa wa shule 104,449 walisajiliwa, wavulana ni 57,378 sawa na asilimia 54.9 na wasichana ni 47, 071 sawa na asilimia 45.1.
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu ni 232 ambapo wenye uoni hafifuni 201, wasioona ni 16 na wenye ulemavu wa viungo vya mwili ni 15.
Dk. Mohamed alisema mtihani wa kidato cha sita utaanza Mei 6 hadi Mei 24, mwaka huu kwa shule za sekondari 931 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 258 na mtihani wa ualimu kwa vyuo vya ualimu 99.
“Kati ya watahiniwa wa Kujitegemea 9,055 walisajiliwa, wavulana ni 5,515 sawa na asilimia 60.91 na wasichana ni 3,540 sawa na asilimia 39.09 huku wenye mahitaji maalumu wakiwa watatu ambao wote wanao uoni hafifu.
Mwaka jana, idadi ya watahiniwa wa shule wa Kujitegemea walisajiliwa walikuwa 106,883 hivyo kuwepo na ongezeko la jumla la watahiniwa 6,621 sawa na asilimia 6.19 kwa mwaka huu,” amesema.
MTIHANI WA UALIMU
Dk.Mohamed amesema jumla ya walimu 12,552 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambapo kati yao watahiniwa 2, 766ni ngazi ya stashahada, wanaume ni 1,634 sawa na asilimia 59.07 na wanawake ni 1,132 sawa na asilimia 40.93.
“Kwa watahiniwa 8,786 wa ngazi ya cheti, jumla ya watahiniwa 3,969 sawa na asilimia 45.17 ni wanaume na 4,817 sawa na asilimia 54.83 ni wanawake,”amesema.
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosajiliwa ni 12 huku wenye uoni hafifu ni wawili kwa ngazi ya stashahada na wanane Kwa ngazi ya cheti huku watahiniwa wasioona Kwa ngazi ya cheti ni wawili.
Ameongeza kuwa mwaka jana idadi ya watahiniwa wa ualimu waliosajiliwa walikuwa 8,479 hivyo Kuna ongezeko la jumla la watahiniwa 3,073 sawa na asilimia 36,24 Kwa mwaka huu.
MAANDALIZI YA MTIHANI
Akizungumzia kuhusu maandalizi Dk. Mohamed amesema maandalizi yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa Mitihani husika,vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu Mitihani hiyo katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
“Kamati za Mitihani za mikoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu na kutoa semina kwa wasimamizi wa Mitihani pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vya Mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,”amesema.
Pia amesema mtihani wa kidato cha sita ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwani hupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi katika maeneo yote waliyojifunza kwa kipindi cha miaka miwili ya elimu ya sekondari ya juu.
“Matokeo ya mtihani huu utumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanajiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati katika fani mbalimbali za utaalam wa kazi kama vile Afya, kilimo, Ualimu, ufundi na nyinginezo .
hivyo mtihani huu ni muhimu sana kwa wanafunzi, wazazi, jamii nzima na taifa kwa ujumla,”amesisitiza.
Baraza hilo limewaomba wananchi wote kutoa ushirikiano wakati wa Uendeshaji wa mitihani ili watahiniwa wote wafanye mtihani katika hali ya utulivu.
Amewataka wananchi wote watoe ushirikiano katika kudhibiti vitendo vyovyote vya udanganyifu katika mtihani wa kidato cha sita na ualimu mwaka huu baraza halitasita kumchukulia mtu atakayebainika kujihusisha na kusababisha udanganyifu kufanyika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Dk. Mohamed amesema limewaasa wakuu wa shule kutekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi uliotolewa na Baraza hilo na kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba.
Aidha, Baraza limewaasa wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum ya mtihani na huvyo hawatakiwu kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mitihani hiyo.