*Aungana na wakazi Dar kufanya mazoezi
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki mazoezi ya pamoja ya kampeni ya kitaifa inayoratibiwa na Wizara ya Afya ya kuhamasisha ufanyaji wa mazoezi kwa watanzania ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua hiyo pia ni kuunga mkono wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa hayo.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi Mei 4, 2024) aliposhiriki katika kampeni ya ufanyaji mazoezi pamoja na matembezi ya kilomita 10 yaliyoanzia katika fukwe za Coco kupitia daraja la Tanzanite hadi Ocean Road jijini Dar es Salaam.
“Mnakumbuka programu hii iliyoanzishwa na Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na yeye mwenyewe kushiriki na kuwahamasisha watanzania kushiriki mazoezi mbalimbali, katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk. Samia moja ya mambo ya kujivunia ni mafanikio katika sekta ya michezo,” amesema Majaliwa.
Kadhalika Majaliwa ametoa wito kwa Viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kufanya maboresho zaidi katika eneo la fukwe za Coco ili liwe safi na livutie watu wa rika mbalimbali.
“Nawapongeza jeshi la polisi kwa kazi nzuri ulinzi katika eneo hili, Nitoe wito kwenu kuendelea kuimarisha ulinzi ili eneo hili liwe salama kwa watu wa rika na jinsia zote,” amesema Majaliwa.
Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kushiriki katika mazoezi hayo huku akitoa taarifa ya ongezeko la magonjwa 10 yasiyo ya kuambukiza jambo lililofanya Wizara hiyo kuleta ombi la kuanzishq utaratibu wa mazoezi kila jumamosi.
“Mwaka 2022 kati ya magonjwa 10 yanayowasumbua watanzania moja lililojitokeza ni shinikizo la juu la damu bajeti ya mwaka 2022/2023 likaongezeka na kisukari katika mahlgongwa 10 yanayowasumbua watanzania. Wajibu wa Wizara ya Afya ni kuwakinga Watanzania wasipate magonjwa,” amesema Ummy.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila amesema kama Mkoa watajipanga kuhakikisha utaratibu huo wa mazoezi utakuwa endelevu kwa kishirikiana na kamati ya Ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.