27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ajifungua pacha wanne Muhimbili

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

MKAZI wa Kimara, Abednego Mafuluka, ameiomba Serikali na jamii kumsaidia malazi ya watoto pacha wanne ambao mkewe, Sara Dimosa, amejifungua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Akizungumza jana na MTANZANIA Jumamosi katika wodi namba 10 ambako mkewe amelazwa, Mafuluka alisema amelazimika kuomba msaada kwa sababu watoto hao wanahitaji matunzo makubwa.

“Mke wangu amejifungua kwa upasuaji watoto wanne Aprili 4, mwaka huu na tuna watoto wengine wawili ambao Mungu ametujalia kwa maana hiyo sasa tuna jumla ya watoto sita na wote wanahitaji matunzo.

“Hawa wawili wakubwa wameanza shule. Tunakoishi tumepanga hivyo natafuta fedha za matunzo ya familia, pango la nyumba na sasa hawa mapacha wanahitaji maziwa ya ziada ili waweze kuishi maana ya mama yao hayatoshi na lazima nipate fedha kwa ajili ya kumnunulia chakula cha kutosha,” alisema Mafuluka.

Alisema kazi yake ni fundi umeme aliyejiajiri mwenyewe na kwamba amekuwa akikutana na changamoto nyingi za ugumu wa maisha licha ya kujituma katika kazi zake.

Naye Sara, mama wa pacha hao alisema anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kujifungua watoto hao wakiwa salama.
“Nashukuru Mungu pia familia zetu zimepokea kwa furaha juu ya watoto wetu na wamekuwa wakitusaidia lakini hatuwezi kuwategemea kila siku. Nitahitaji na wasichana wa kunisaidia ambao nitatakiwa kuwalipa mshahara hivyo nalazimika kuomba jamii nayo itusaidie,” alisema Sara.

Kwa upande wake, nesi msaidizi wa wodi hiyo, Enessy Mwambene, alisema watoto hao wamezaliwa bila tatizo lolote na wanaendelea vizuri hadi hivi sasa.

“Muhimbili tunajisikia fahari kwa kufanikisha upasuaji huu umepita muda mrefu kupokea mama aliyejifungua watoto wanne, ni vyema wasamaria wema wakajitokeza kuisaidia familia hii kulea watoto wao kama inavyopaswa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles