27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kashfa ya Panama yamtesa Cameron

david_cameron_0NA MWANDISHI WETU

KASHFA kubwa ya ukwepaji kodi iliyoibuliwa hivi karibuni ikifahamika zaidi kama ‘Panama Papers’ ambayo inawagusa baadhi ya viongozi na wafanyabiashara wa mataifa makubwa na madogo duniani imeanza kumtesa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.

Taarifa za nyaraka hizo za siri zilivuja kutoka katika chanzo kisichojulikana mwishoni mwa wiki na kunaswa na Jopo la Kimataifa la Wanahabari Wapekuzi (ICIJ) ambao walianza kusambaza katika vyombo mbalimbali vya habari duniani kote kwa kutumwa kwa waandishi wa habari 370 na vyumba vya habari 107.

Kashfa hiyo imewagusa marais na viongozi wakuu wengi walioko madarakani kwa sasa akiwemo Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Xi –Jinping wa China.

Katika kashfa hiyo, David Cameron, amenaswa kwa kuwa mwanahisa wa Kampuni ya Blairmore Holding Inc ambayo imehifadhi fedha kwa siri katika taasisi za kifedha nchini Panama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa jana katika gazeti la The Guardian la nchini Uingereza, Cameron amekiri kwamba amewahi kunufaika na kampuni hiyo wakati akiwa mwanahisa lakini aliuza hisa zake miezi michache kabla ya kuwania Uwaziri Mkuu mwaka 2010.

Cameron amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kubainika kuwa kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na baba yake mzazi, Ian Cameron, imekwepa kodi nchini Uingereza kwa takribani miaka 30.

Kampuni hiyo iliyokuwa inajihusisha na masuala ya uwekezaji wa kifedha nchini Panama, inatajwa kuwa awali ilificha fedha zake nchini Uswisi.

Katika maelezo yake aliyoyatoa juzi usiku kwenye kituo cha televisheni cha ITV cha nchini Uingereza, Cameron alisema kwamba aliwekeza hisa zenye thamani ya Paundi 30,000 sawa na Sh milioni 90 na miezi minne kabla ya kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza aliuza hisa zake.

Alisema hisa zake aliziuza kwa Paundi 31,500 sawa na Sh milioni 95 katika kampuni moja iliyosajiliwa nchini Bahama. Hata hivyo, Cameron alisisitiza kuwa alilipa kodi ya mapato kutokana na mgawo wa mauzo ya hisa hizo alizonunua mwaka 1997.

Katika hatua nyingine, Cameron alikiri wazi kuwa hajui kama Paundi 300,000 sawa na Sh milioni 900.4 alizorithi kutoka kwa baba yake mzazi zilitokana na kukwepa kodi ya nchi hiyo.

“Kawaida siwezi kunyooshea kidole chanzo cha kila fedha ya baba yangu na baba hayupo kwa ajili yangu kumuuliza maswali sasa,” alisema Cameron.

Tayari kashfa hiyo imezua mtafaruku mkubwa kiasi cha kumtikisa Waziri Mkuu wa Iceland, Sigmundur Gunnlaugsson ambaye awali alijiuzulu baada ya kutajwa kuwa ni miongoni mwa viongozi waliokwepa kodi na kutakatisha fedha.

Tangu Jumapili iliyopita usiku, vyombo vya habari duniani kote vilianza kuchapisha taarifa kuhusu mali zilizofichwa na viongozi mbalimbali kutoka duniani kote.

Viongozi wengine ambao wanashikilia madaraka kwa sasa wametajwa katika nyaraka hizo za siri ambazo zimetumwa kwa mamia ya wanahabari duniani kote.

Nyaraka hizo nyingi ambazo zina barua pepe, maelezo na fax, zimetolewa na chanzo ambacho hakikutajwa jina katika gazeti la kila siku la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung na magazeti mengine ikiwamo nchi ya Uingereza.

Gazeti hilo la Ujerumani na yale ya Uingereza  yameshirikiana na vyumba vya habari vingine 106 duniani kote na kwa makubaliano na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari wanaojihusisha na utafiti mjini Washington nchini Marekani.

Tangu Jumapili, Aprili 3, magazeti hayo yamekuwa yakichapisha taarifa ambazo zinaweza kuwa ngumu kwa baadhi ya viongozi duniani.

Wakuu wa nchi 12 duniani ikiwa ni pamoja na sita ambao bado wanashikilia madaraka wamewekwa hatarini.

Pia kuna mabilionea ambayo yamebainiwa kuhifadhiwa na vigogo katika michezo kama vile mchezaji wa soka, Lionel Messi na Michel Platini. Inaelezwa kuwa wote wanaaminika kuwa walitumia ujanja wa ‘offshore’ kwa kuficha mali zao.

Miongoni mwa majina yaliyotajwa mbali na  Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, yupo Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Nawaz Sharif.

Wengine ni Mfalme wa Saudi Arabia Salman, Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko, mwenzake wa Argentina, Mauricio Macri, na Waziri Mkuu wa Iceland, Sigmundur Gunnlaugsson ambaye tayari ametangaza kuondoka madarakani kwa shinikizo la wananchi wake lakini pia akikiri kushindwa kuweka wazi mali anazomiliki mkewe.

Pia watu wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, nao wanakabiliwa na kashfa hiyo.

Kwa upande wa Bara la Afrika ukimuacha Rais pekee wa zamani wa Sudan al-Mirghani, aliyefariki mwaka 2008 ambaye amehusishwa moja kwa moja katika kashfa hii, pia kuna watu wa karibu wa viongozi sita kama mpwa wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, mjane wa Rais wa zamani wa Guinea, Lansana Conte na katibu binafsi wa mfalme wa Morocco.

Mawaziri kadhaa na viongozi waandamizi pia wametajwa, ikiwa ni pamoja na Mbunge na dada wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Kongo, Jaynet Kabila Kyungu, Waziri wa Viwanda na Madini wa Algeria, Emmanuel Ndahiro.

Wengine ni mkuu wa zamani wa Idara ya Ujasusi nchini Rwanda, Bruno Jean na Richard Itoua ambaye ni Waziri wa utafiti wa Congo-Brazzaville.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles