24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Masikini Kitilya, Miss Tanzania

Pg 1*Wakosa dhamana, warudishwa rumande

*Pia yumo mtoto wa waziri

 

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

KAMISHNA Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon, wanaendelea kusota rumande baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali maombi yao ya dhamana.

Maombi hayo yalitupwa jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru, wakati kesi yao ilipokuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa maombi hayo.

Akitoa uamuzi wa maombi hayo, Hakimu Mchauru, alisema amekubaliana na hoja za upande wa mashtaka kwamba shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Alisema katika kufikia uamuzi huo pia amekubaliana na hoja iliyotolewa na upande wa mashtaka kuhusiana na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ilipoketi kama Mahakama ya Kikatiba kwamba makosa ya utakatishaji fedha yana athari kiuchumi.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, upande wa utetezi uliwasilisha hoja nyingine ya kupinga shtaka hilo la utakatishaji dhidi ya washtakiwa hao kwa madai kwamba halijakidhi matakwa ya kisheria.

Akiwasilisha hoja hizo kwa niaba ya utetezi, Wakili Alex Mgongolwa, alidai wanapinga shtaka hilo kwa madai kuwa kosa hilo halijabainisha jinsi washtakiwa walivyotenda na inatakiwa lioneshe wazi.

“Ili kosa la utakatishaji lisimame lazima lisimame katika kifungu 12 (a hadi e) cha sheria ya makosa ya utakatishaji na sio kifungu 12 (a) pekee kama ilivyo katika hati ya mashtaka, hivyo ni rai yetu tunaomba shtaka hili liondolewe,” alidai Mgongolwa.

Alidai kuwa ili kosa hilo lionekane lazima lihusishe hatua nne muhimu ikiwemo chanzo kichafu cha upatikanaji wa fedha hizo.

Naye Wakili wa utetezi, Majura Magafu, alidai kuwa kifungu namba 234 cha sheria ya kanuni ya adhabu kinaipa mamlaka upande wa mashtaka kufanyia marekebisho hati ya mashtaka inapoona haijakidhi vigezo vya kisheria ila kwa zile dosari ndogondogo tu.

Alidai kwamba kutokana na hali hiyo ni vyema upande wa mashtaka ukaiomba mahakama kurekebisha hati yao ya mashtaka.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekoma, aliomba mahakama itupe hoja za utetezi kwa kuwa hazina mashiko kisheria.

Alidai kwamba kifungu namba 12 (a) cha makosa ya utakatishaji kinasimama chenyewe na si lazima matendo yote yaliyosababisha kutendeka kosa hilo yaorodheshwe katika hati ya mashtaka.

“Shtaka hili linaelezea namna na jinsi walivyojihusisha katika muhamala kama sheria inavyotaka, kwa maana hiyo ni hoja yetu shtaka la utakatishaji fedha libaki kama lilivyo na hoja za upande wa utetezi zitupwe,” alidai Tibabyekoma.

Baada ya kuwasilishwa kwa hoja hizo, Hakimu Mchauru, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, mwaka huu atakapotoa uamuzi na washtakiwa wote walirudishwa rumande katika Gereza la Keko.

Washtakiwa hao katika kesi hiyo, Kitilya, Shose aliyewahi kuwa Mrembo wa Tanzania mwaka 1996 na Sioi aliyewahi kugombea ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki mwaka 2012 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya baba yake aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari, kufariki dunia, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kupandishwa kizimbani Aprili mosi, mwaka huu wakikabiliwa na jumla ya mashtaka nane likiwamo la utakatishaji wa dola milioni sita za Marekani sawa na zaidi ya Sh bilioni 12 ambazo ni mali ya Serikali ya Tanzania.

Mashtaka yao yanatokana na tuhuma za ufisadi zilizowahi kuibuka baada ya Serikali ya Tanzania kudaiwa kupoteza zaidi ya Sh trilioni 1.3 katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2013 wakati ikiuza hati fungani zake kwa Benki ya Stanbic inayomilikiwa na Standard Group ya Afrika Kusini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles