NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
IKIWA imebaki siku moja kabla ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kushuka dimbani kuikabili Al Ahly katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, amesema kuwa yupo tayari kukubali matokeo yoyote watakayoyapata uwanjani.
Yanga, ambayo imeweka kambi Kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo huo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya kimataifa, inatarajiwa kurejea jijini leo, huku wapinzani wao kutoka Misri tayari wameingia nchini juzi alfajiri.
Mchezo kati ya timu hizo umepangwa kuchezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kesho, kabla ya timu hizo kurudiana jijini Cairo, Misri siku 10 baadaye.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Pluijm alisema kwa upande wake tayari mafunzo na maelekezo yote kwa wachezaji yamekamilika, hivyo anasubiri mchezo huo ufanyike.
Pluijm alisema yamezungumzwa mengi kipindi hiki cha maandalizi, ila anaamini wachezaji wake hawatamuangusha kwa kufanya makosa yatakayopelekea timu hiyo kufungwa kirahisi.
“Nasubiri dakika 90 ziamue nani mshindi, siwezi kuzungumza sana, kwani tayari kila kitu kimekamilika na wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri na morali ya hali ya juu.
“Kila timu imejiandaa kwa upande wake, ndiyo maana ninasema nipo tayari kukubaliana na matokeo yoyote, ingawa malengo yetu makubwa ni kushinda nyumbani na ugenini.
“Nafahamu hawa wenzetu watakuwa wamejiwekea mikakati yao, ila hata sisi tumefanya maandalizi ya kutosha na kila mwalimu anategemea kikosi chake kiibuke na ushindi,” alisema Pluijm.
Mholanzi huyo alieleza matarajio yake makubwa ni kuishuhudia Yanga ikiiondosha Al Ahly kama ilivyokuwa kwa timu za nyuma na kusonga mbele katika hatua ya nane bora ya michuano hiyo.