23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

CUF wamwangukia Rais Magufuli umeya Tanga

Magdalena Sakaya_NECNA NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati mgogoro wa umeya wa Jiji la Tanga   kuruhusu kuanza vikao vya Baraza la Madiwani na kuharakisha shughuli za maendeleo za jiji hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya, alisema   Dar es Salaam jana kuwa madiwani wao wameamua shughuli zote za baraza la madiwani zisiendelee mpaka mgogoro huo utakapotatuliwa.

Alisema katika uchaguzi uliofanyika Desemba 19 mwaka jana, CUF ilikuwa na madiwani 20 huku CCM ikiwa na madiwani 17.

Baada ya kupiga kura na kuhesabiwa kwa kuthibitishwa na mawakala wa wagombea, mgombea wa CUF, Rashid Jumbe, alipata kura 20 na Selemani Mustafa wa CCM  alipata kura 17.

“Lakini wakati wa kutangaza matokeo, mkurugenzi alitangaza tofauti na  kumtangaza mgombea wa CUF kuwa alipata kura 18 na wa CCM kura 19.

“Jambo hilo lilipingwa na wakala wa mgombea wetu ambaye na kuwasilisha hoja ya kutaka kura zihesabiwe tena lakini mkurugenzi alikimbia na sanduku la kura na  kujifungia ofisini.

“Uporaji huu hauvumiliki na haukubaliki, hatuko tayari kuacha jiji hili liongozwe na meya asiye halali na aliyepora demokrasia kwa masilahi yake binafsi na wenzake.

“Hivyo tunamuomba Rais Magufuli atumie busara zilezile zilizosaidia kumaliza mgogoro wa umeya wa Dar   kuharakisha shughuli za maendeleo za jiji la Tanga,” alisema Sakaya.

Alisema walifanya jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kukutana na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza na Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Tunasikitishwa sana na namna shughuli za maendeleo zinavyokwama kwa sababu ya kikundi kidogo cha watu kuamua kuchezea demokrasia na kukataa kutoa haki kwa wananchi wa Tanga,” alisema.

Naye Mbunge wa Tanga mjini kupitia chama hicho, Musa Mbarouk, alidai   wamekuwa wakifanyiwa hujuma mbalimbali zikiwamo kubambikiwa kesi   washindwe kufanya shughuli za  siasa.

Mbunge huyo alishauri vikao vya baraza la madiwani viendelee kwa kusimamiwa na naibu meya ambaye alipatikana kwa halali wakati wakiendelea kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Alipoulizwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema kama pande zinazosigana hazitaki kuelewana   halmashauri hiyo itafutwa.

“Hoja za CUF hazina maelezo ya msingi, mbona katika matokeo ya naibu meya kura moja ilizidi, sasa inashindwaje kutokea katika nafasi ya umeya?

“Kama wanaona kulikuwa na ukiukwaji mwingine wa sheria waende mahakamani lakini huwezi kuyabadili matokeo kwa maneno,” alisema Simbachawene.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles